Balozi wa Kuwait nchini ,Mhe.Jasem Al- Najem akizungumza na baadhi ya wananchi wa Vigwaza kwenye zahanati ya Vigwaza Chalinze Bagamoyo Mkoani Pwani baada ya kumkabidhi diwani wa kata ya Vigwaza Mohsin Bharwani vifaa vya watu wenye ulemavu na mabeseni 100 yenye vifaa vya uzazi vyote vikiwa na thamani ya mil.17.5.(picha na Mwamvua Mwinyi)
Balozi wa Kuwait nchini ,Mhe.Jasem Al- Najem wa kwanza
kushoto akikabidhi vifaa vya watu wenye ulemavu na mabeseni 100 yenye vifaa vya
uzazi vyote vikiwa na thamani ya mil.17.5,
Kwa diwani wa kata ya Vigwaza Mohsin Bharwani wa
pili kutoka kulia.
picha na Mwamvua Mwinyi
Na Mwamvua Mwinyi,Vigwaza
Balozi wa Kuwait nchini ,Mhe.Jasem Al- Najem amemkabidhi
diwani wa kata ya Vigwaza ,jimbo la Chalinze Bagamoyo mkoani Pwani ,Mohsin
Bharwani vifaa vya watu wenye ulemavu na mabeseni 100 yenye vifaa vya uzazi
vyote vikiwa na thamani ya mil.17.5.
Kati ya fedha hiyo kiasi cha sh.mil .13 ni
gharama ya vifaa vya watu wenye ulemavu ikiwemo magongo 20,fimbo za wenye
ulemavu 10,fimbo za walemavu wa macho 10,miwani 20 ,mafuta ya wenye ulemavu wa
ngozi na viti vya kubebea wagonjwa kwa watu wazima 20 na kwa watoto kumi.
Pamoja na hilo ,sh mil.4.5 ni gharama ya mabeseni 100 yenye
vifaa vya akinamama wajawazito kabla na baada ya kujifungua .
Akipokea vifaa hivyo,kwenye zahanati ya Vigwaza ,diwani wa
kata ya Vigwaza Bharwani alimshukuru balozi wa Kuwait nchini Al-Najem na kusema
ni balozi wa mfano na anastahili kuigwa .
Alieleza wamekuwa wakishuhudia misaada mingi ikielekezwa
mijini lakini balozi huyo amefika kijijini kwa watu wenye shida na wanaohitaji
misaada kama hiyo.
Aidha aliwaomba mabalozi wengine waende kwenye kata hiyo
,kuwezesha na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili
"Nilionana na mdau Muntazir Hussein ambae alikuwa kiungo
wa kunisaidia kunikutanisha na balozi Al-Najem " alisema Bharwani.
Hata hivyo ,Bharwani alimshukuru balozi huyo kwa jitihada
zake za kuwaunga mkono ,kwa niaba ya serikali ya Kuwait na Red Cross Society ya
Kuwait kwa msaada huo ambao utawasaidia akina mama wajawazito na wenye ulemavu.
Akikabidhi vifaa hivyo,balozi wa Kuwait nchini Al-Najem
alisema amekabidhi vifaa Kwa ajili ya watu wenye ulemavu vyenye thamani zaidi
ya dola 6,000 sawa na sh.mil.13 na vifaa vya uzazi mil.4.5.
Alisema mpango huo ulianza kwa kumkabidhi Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan vifaa tiba vya uzazi
ambavyo vitasambazwa katika hospitali mbalimbali kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema Serikali ya nchi hiyo kwa ushirikiano na Red Cross
Society ya Kuwait imetoa vifaa hivyo kama hatua ya kuendelea kudumisha na
kuendeleza mahusiano mazuri kati ya nchi hiyo na Tanzania.
Al- Najem alielezea serikali ya Kuwait itaendelea
kusaidia Serikali ya Tanzania katika uimarishaji wa sekta ya afya na elimu
nchini .
Alisisitiza vifaa hivyo vifikishwe kwa walengwa ili vilete
tija kwa maslahi ya jamii.
Akimshukuru balozi wa Kuwait nchini Tanzania kwa niaba ya
wananchi, mwenyekiti wa kijiji cha Vigwaza ,Ramadhani Kirumbi alimpongeza pia
diwani kwa kujitoa kutafuta wadau Kwa ajili ya wakazi wa Vigwaza.
Alisema licha ya kupokea vifaa hivyo lakini zahanati ya
Vigwaza bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maabara,jengo la watoto na
wodi ya akina baba.
Kirumbi alisema endapo changamoto hizo zitatatuliwa
itawezesha zahanati hiyo kuwa kituo cha afya.
Alimuomba balozi wa Kuwait asichoke kuwashika mkono na
kuendelea kuwaunga mkono kwa changamoto nyingine zinazowagusa.


0 Comments