Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
(aliyesimama) akizungumza na Wafanyakazi, Wachimbaji na Wafanyabiashara wa
Madini ya Jasi (hawapo pichani) wakati wa ziara yake Itigi Mkoani Singida.
Kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Pius Luhende.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
(katikati) akitembelea Kiwanda cha kutengeneza Chaki cha Furaha, kilichopo
katika Kata ya Tambukareli, Itigi. Kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Itigi, Pius Luhende na kushoto ni Meneja wa Kiwanda hicho, Peter Nolasco.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia)
akizungumza jambo alipotembelea Kiwanda cha kuzalisha Chaki cha Dobercolor
kilichopo katika Kijiji cha Majengo, Itigi. Wengine ni baadhi ya wafanyakazi wa
Kiwanda hicho.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo
(katikati) akimsikiliza Meneja wa kiwanda cha kuzalisha Chaki cha Furaha, Peter
Nolasco (kushoto). Kutoka kulia ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati
Singida, Sosthenes Massola na Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Madini wa
Mkoa wa Singida (SIREMA), Farijala Kiunsi.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Mapambo ya
majumbani cha RSR kilichopo Singida Mjini, Rashid Rashid (kushoto) akimuonesha
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) baadhi ya bidhaa
zinazozalishwa kiwandani hapo zitokanazo na Madini ya Jasi yanayochimbwa Itigi
mkoani humo.
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Singida,
Sosthenes Massola (kushoto) akizungumza na Wafanyakazi, Wachimbaji na
Wafanyabiashara wa Madini ya Jasi (hawapo pichani) wakati wa ziara ya Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia aliyesimama) Mkoani Singida.
.............
Wachimbaji
wa Madini ya Jasi Mkoani Singida wametakiwa kufanya shughuli zao kwa uaminifu
ili kujihakikishia soko la uhakika.
Naibu
Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa wito huo Desemba 11, 2017 Wilayani Itigi
mara baada ya kuzungumza na Wachimbaji wa madini hayo wakati wa ziara yake kwenye
maeneo yenye uchimbaji wa madini ya Jasi Mkoani Singida.
Wachimbaji
wa Madini hayo walimueleza Naibu Waziri Nyongo changamoto mbalimbali
zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa soko la uhakika.
Mara
baada ya wachimbaji hao kuelezea changamoto zinazowakabili, Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Itigi, Ali Minja alimueleza Naibu Waziri Nyongo kwamba tatizo la
soko la Madini ya Jasi yanayochimbwa Singida linasababishwa na wachimbaji
wenyewe kwa kuchanganya madini hayo na udongo.
Alisema
wakati mwingine wachimbaji wenyewe wanasababisha kupotea kwa soko, kwani
mnunuzi akinunua Madini ya Jasi yaliyochanganywa na udongo hawezi kurudi tena
kununua.
“Baadhi
ya wachimbaji wa Jasi Mkoani hapa sio waaminifu kwani wanachanganya madini na takataka
ikiwemo udongo, na hii inakimbiza wanunuzi,” alisema.
Kufuatia
hali hiyo, Naibu Waziri Nyongo aliwaasa wachimbaji hao kuwa wakweli kwa kufanya
shughuli zao kwa uadilifu na ubunifu mkubwa wa utafutaji wa masoko ili kuvutia
wanunuzi wengi zaidi na hivyo kujiongezea kipato.
Alisema
mafanikio hayawezi kupatikana kama wachimbaji watafanya shughuli zao kwa
ulaghai na aliwataka kuacha kutafuta mafanikio kwa njia ya mkato ikiwemo hiyo
ya kuchanganya Jasi na takataka ambayo alisema imewasababishia kukimbiwa na
wanunuzi.
“Tukitumia
madini haya vizuri huku tukiongeza ubunifu, tutafanikiwa kufikia malengo
tuliyojiwekea; vinginevyo tutaendelea kulalamika,” alisema.
Aliongeza
kwamba Serikali itafanya jitihada za kutangaza Madini ya Jasi yanayochimbwa
nchini na kuwataka wachimbaji wa madini hayo kuhakikisha wanazingatia suala la
ubora unaotakiwa Kimataifa.
“Ninawahakikishia
tutawatafutia soko mahala popote Duniani, ili kuhakikisha mnanufaika na madini
haya mnayochimba ila mkumbuke uaminifu ni muhimu,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Aidha,
aliongeza kwamba Serikali inakaribisha wawekezaji wakubwa kuwekeza kwenye
biashara ya Madini ya Jasi ikiwemo ujenzi wa viwanda vinavyotumia Madini ya
Jasi kama malighafi ya kutengenezea saruji na bidhaa mbalimbali kama mapambo ya
majumbani na chaki.
Naibu
Waziri Nyongo yupo Mkoani Singida kwa ziara ya siku tatu ya kutembelea shughuli
za uchimbaji wa Madini mkoani humo pamoja na kuzungumza na wachimbaji ili
kubaini changamoto zinazowakabili kwa lengo la kutafutia ufumbuzi.
0 Comments