Naibu
Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge
wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde (wa pili kushoto) akizungumza katika
mkutano na Wafanyabiashara wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma baada
ya Vibanda vyao kubomolewa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO)
kupisha mradi wa ujenzi wa Reli kisasa. Kulia ni Naibu Meya wa Manispaa
ya Dodoma Jumanne Ngede na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri
hiyo Godwin Kunambi. Kushoto ni Katibu wa Wafanyabiashara hao John
Banda.
Baadhi
ya wafanyabiashara wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma wakifuatilia
mkutano wao na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde, Naibu Meya wa
Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo
Godwin Kunambi.
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (wa pili kushoto)
akiteta jambo na wafanyabiashara wakati akitoka katika eneo la Stendi ya
Jamatini Mjini Dodoma baada ya kuzungumza na wafanyabiashara
waliovunjiwa vibanda vyao kupisha mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa.
......
HALMASHAURI ya Manispaa
ya Dodoma inatarajia kuwapatia eneo wafanyabiashara zaidi ya 550 waliovunjiwa
vibanda vyao na kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) katika stendi ya
mabasi madogo ya Jamatini ili kupisha utekelezaji wa mradi wa Reli ya
kisasa, ili waendelee kufanya biashara zao kama kawaida.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amewaeleza wafanyabiashara hao
kuwa, Manispaa iko katika hatua za mwisho kuandaa eneo la Makole D-Center kwa
kuweka miundombinu muhimu ikiwemo mfumo wa maji safi na maji taka ili
wafanyabiashara hao waanze kufanya shughuli zao mara moja na katika mazingira
rafiki na salama katika eneo hilo.
Aliyasema hayo
alipotembelea eneo la Jamatini na Stendi Kuu Novemba 6 mwaka huu, akiambatana
na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira Anthony Mavunde
ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, pamoja na Naibu Meya wa Halmashauri ya
Manispaa hiyo Jumanne Ngede kwa lengo la kuwapa pole wafanyabiashara hao na
kuwajulisha hatua zilizochukuliwa na Viongozi mbalimbali katika kuhakikisha
tatizo linalowakabili linapatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Aliwatoa hofu ya kuwa
eneo hilo halitakuwa na wateja wengi kama ilivyokuwa eneo la stendi ya
Jamatini, ambapo aliwaambia tayari Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith
Mahenge ametoa maelekezo kwa Manispaa na Sumatra kuhakikisha daladala zinakuwa
na ruti inayopita katika eneo hilo jipya la biashara ambapo abiria watakuwa na
kituo cha kupanda na kushuka na hivyo kuongeza mzunguko wa wateja katika eneo
hilo, na kwamba utekelezaji wa maelekezo hayo umeshaanza kufanyiwa kazi na
Sumatra.
Akizungumza na
wafanyabiashara ya usafiri wa mabasi katika Stendi Kuu ya mabasi ya mikoani,
Mkurugenzi Kunambi aliwaambia kuwa, Manispaa kwa kushauriana na uongozi wa Mkoa
na wadau kama Sumatra imepanga kuhamishia Stendi hiyo katika eneo la Chaduru au
kwenye eneo la viwanja vya Nanenane vilivyopo Kata ya Nzuguni barabara kuu ya
Dodoma-Dar es Salaam.
Alisema Manispaa
itazungumza na uongozi wa wasafirishaji ili kupata mapendekezo yao juu ya
eneo rafiki zaidi miongoni mwa maeneo hayo mawili.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri Mavunde aliwataka wote walioathiriwa na zoezi hilo la bomoabomoa wawe
watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Mamlaka na Viongozi wakifanya juhudi
za makusudi kuwatafutia maeneo rafiki kwa shughuli zao huku Naibu Meya Ngede
akiwahakikishia kuwa Baraza la Madiwani litasimamia kikamilifu suala la
upatikaaji wa maeneo hayo.



0 Comments