NA TIGANYA Vincent RS TABORA
JUMLA ya ng’ombe na punda 198,681 wamepigwa chapa katika Halmashauri ya Sikonge hadi kufikia sasa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali.
Kiwango hicho ni sehemu ya matarajio ya Halmashauri hiyo ya kupiga chapa punda na ng’ombe 249,000 hadi mwisho wa zoezi hilo.
Zoezi hilo lililoanza mapema Desema mwaka jana lilihusisha upigaji chapa ng’ombe 198,634 na punda 47.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya zoezi ya chapa ya ng’ombe na punda katika Wilaya ya Sikonge, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri aliwaagiza Maofisa Mifugo na Uvuvi katika Wilaya zote kuhakikisha hakuna ng’ombe wala punda atakayesalia katika eneo bila chapa.
Alisema kuwa zoezi hilo licha faida za kudhibiti wizi, magonjwa na kusaidia katika mpango wa matumizi bora ya ardhi , utausaidia Mkoa kupambana na uvamizi wa makundi makubwa ya ng’ombe kutoka katika mikoa mingine.
Mwanri alisema kuwa makundi hayo ndiyo yamekuwa yakisababisha ubaribifu katika hifadhi mkoani humo na kusababisha ukame.
Alisema kuwa baada ya siku ya mwisho kumalizika Maofisa Mifugo na Uvuvi waanze kufuatilia ili kuona kama Mifugo ambayo itakuwa haina chapa kwa ajili wahusika kuchukualiwa hatua ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya Sheria kwa hatua zaidi.
Naye Kaimu Ofisa Mifugo na Uvuvi Mipawa Majebele kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge alisema kuwa hatua hiyo itasaidia Mkoa wa Tabora kuwa utambuzi na ufuatiliaji Mifugo kupitia usajili wa mifugo yenyewe, wamiliki wake, mahali ilipo na matukio muhimu kwenye uhai wa mifugo hiyo.
Alisema kuwa zoezi hilo litawasaidia wafugaji kupangiwa maeneo ya kuchingia kulingana na Wilaya husika na kuwa na uwezo wa kuanzisha vyama vyao vya ushirika.
Majebele aliongeza kuwa zoezi hilo litasaidia kuzuia magonjwa ya mifugo kutoka eneo moja kwenda jingine na itakuwa rahisi kwa wataalamu wa eneo husika kutoa chanjo na ujenzi wa majosho.

0 Comments