Serikali
imetoa onyo kali kwa waliojinufaisha na kutumia ruzuku ya uchimbaji madini
kinyume na makusudio yake ambao hadi sasa hawajarejesha licha ya kutakiwa
kufanya hivyo.
Naibu
Waziri wa Madini, Doto Biteko alitoa onyo hilo Februari 26, 2018 kwenye mkutano
na wananchi na wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Isanga, Kata ya
Lusu Wilaya ya Nzega.
Awali
kabla ya kutoa onyo hilo, wachimbaji hao waliiomba Serikali kuwapatia ruzuku
ili iwasaidie katika shughuli zao za uchimbaji madini ndipo Naibu Waziri Biteko
alipoweka bayana suala hilo la ruzuku.
Alisema
Serikali ilisimamisha utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini
baada ya kubaini kwamba imeshindwa kuleta mafanikio yaliyokusudiwa na kwamba
ilikwishaagiza wale wote waliojipatia ruzuku na kuitumia kinyume na makusudio
wanapaswa kuirejesha mara moja vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
“Wapo
ambao tayari wameanza kurejesha na wengine bado hawajafanya hivyo.
Ninawahakikishia wale ambao bado, tutawachukulia hatua kali za kisheria,”
alisema Biteko.
Alisema
haiwezekani watu wachache wasiokuwa na huruma kwa wanyonge wakatumia fedha ya
Watanzania kinyume na makusudio yake.
Biteko
alisema kuwa lengo la Serikali la utoaji wa ruzuku lilikuwa ni kuhakikisha
wachimbaji wadogo wa madini nchini wanaweza kuendeleza machimbo yao kwa kufanya
shughuli zenye tija kwao na Taifa kwa ujumla hata hivyo, makusudio hayo
hayakufikiwa kama ilivyotarajiwa.
Alibainisha
kuwa Serikali inakuja na mpango mwingine wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata
manufaa kutokana na shughuli zao lakini sio kuwapatia fedha kama ilivyokuwa
hapo awali. “Tunanunua vifaa vya uchimbaji ambavyo vitatumika kuwasaidia na sio
kuwapatia fedha,” alisema Biteko.
Aidha,
Biteko aliwataka wachimbaji kote nchini kujiunga kwenye vikundi ili kujipatia
manufaa mbalimbali ikiwemo urahisi wa kupata huduma za kifedha, kukopesheka na
kuelimishwa njia bora na sahihi ya uchimbaji.
Alisema
wachimbaji watakapojiunga wataweza kuwa na uchimbaji wenye tija na hivyo kutoa
ajira nyingi kwa Watanzania wenzao, kulipa ushuru na tozo mbalimbali za
Serikali na hivyo kujiletea maendeleo wao binafsi lakini pia maendeleo kwa
Taifa kwa ujumla.
Katika
ziara hiyo, Naibu Waziri Biteko aliambatana na mwenyeji wake Mbunge wa Jimbo la
Nzega Vijijini na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala ambapo
walitembelea maeneo ya Chuo cha Dodoma Kampasi ya Nzega (MRI) ambapo zamani
palikuwa ni mgodi wa Reolute.

0 Comments