Mhandisi Khalid
Songoro wa kandarasi ya Songoro Marine Transport Boatyard akimuonesha Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Mhandisi Atashasta Nditiye mchoro wa meli mpya inayojengwa na kampuni hiyo kwa
ajili ya kusafirisha abiria na mizigo kwenye mwambao wa ziwa Nyasa wakati wa
ziara yake kwenye bandari ya Itungi iliyopo Kyela mkoani Mbeya
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye (hayupo pichani) akikagua muonekano wa mpya inayojengwa na
kandarasi ya Songoro Marine Transport Boatyard kwa ajili ya kusafirisha abiria
mia mbili na mizigo tani mia mbili kwenye mwambao wa ziwa Nyasa wakati wa ziara
yake kwenye bandari ya Itungi iliyopo Kyela mkoani Mbeya
Kapteni wa meli Bwana
Noel Madete akimuonesha Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye vifaa vya kisasa vya uendeshaji wa meli vilivyopo kwenye meli
ya mizigo ya MV Njombe wakati wa ziara yake kwenye bandari ya Kiwira iliyopo
wilayani Kyela mkoani Mbeya. Anayeshuhudia aliyevaa koti ni Meneja wa bandari
za ziwa Nyasa Bwana Ajuaye Msese
Muonekano wa meli ya mizigo
ya MV Njombe inayosafirisha mizigo ndani ya ziwa Nyasa kwa wateja wa ndani na
nje ya nchi ikiwa kwenye bandari ya Kiwira iliyopo wilaya ya Kyela mkoani Mbeya
baada ya kukaguliwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi
Atashasta Nditiye (hayupo pichani) wakati wa ziara yake bandarini hapo
Muonekano wa meli ya
MV Songea iliyopo bandari ya Itungi, Kyela mkoani Mbeya baada ya kukaguliwa na
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) ambayo itafanyiwa
tathmini ya gharama za matengenezo na Songoro Marine Transport Boatyard kwa
ajili ya kukarabatiwa na ili ianze kutoa huduma za usafirishaji
Serikali inajenga meli
mpya ya kusafirisha abiria na mizigo ambapo ujenzi wake unagharimu shilingi
biloni tisa kwa ajili ya bandari za Ziwa Nyasa ambapo itatoa huduma kwa
wananchi waishio eneo la mwambao wa bandari za Ziwa Nyasa.
Hayo yameelezwa na
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara yake ya kukagua
maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo kwenye bandari ya Itungi iliyopo wilayani
Kyela mkoani Mbeya yenye uwezo wa kubeba abiria mia mbili pamoja na mizigo tani
mia mbili.
Wakati akitoa taarifa
ya maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo kwa Mhandisi Nditiye, Meneja wa Bandari za
Ziwa Nyasa Bwana Ajuaye Msese amesema kuwa ujenzi wa meli hiyo umegharimu kiasi
cha gharama ya shilingi bilioni tisa na umekamilika kwa kiwango cha asilimia
sabini ambapo ujenzi wake ulianza mwezi Julai mwaka 2017 na utakamilika mwezi
Juni mwaka huu.
Ameongeza kuwa meli
hiyo itaanza kutumika mwezi Agosti mwaka huu na itafanya safari zake kwenye
bandari za ziwa Nyasa kwa wananchi wa mwambao wa ziwa hilo kuanzia bandari ya
Itungi iliyopo wilayani Kyela mkoani Mbeya hadi Bamba bay, Malawi. Msese amesema
kuwa meli hiyo inajengwa na mkandarasi mzawa wa Kampuni ya Songoro Marine
Transport Boatyard.
Mhandisi Nditiye
amesema kuwa Serikali imetoa fedha kujenga meli hiyo mpya ili kutimiza ahadi ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambayo
ameitoa kwa wananchi waishio kwenye mwambao wa ziwa Nyasa.
“Ni matarajio ya
Serikali kuwa meli hii itainua uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla, itaondoa
changamoto ya usafiri, itapunguza gharama ya usafiri kwa kuwa usafiri wa meli
ni wa gharama nafuu sana, hivyo nitoe rai kwa wafanyabiashara watumie meli hii
kusafirisha mizigo yao”, amesema Mhandisi Nditiye.
Pia amelielekeza
Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kufunga mitambo ya kisasa ya mawasiliano kwenye
meli hiyo ili abiria wapate mawasiliano muda wote ndani ya meli wakiwa safarini
ndani ya ziwa Nyasa na nchi za jirani za Malawi na Msumbiji ambapo meli hiyo
itatoa huduma ya usafiri.
Katika ziara hiyo
wilayani Kyela, mkoani Mbeya, Mhandisi Nditiye amekagua meli mpya za kisasa za
MV Njombe na MV Ruvuma kwa ajili ya kubeba mizigo zilizopo kwenye bandari ya
mizigo ya Kiwira.
Bwana Msese amesema kuwa meli hizo zimeanza kazi ya
kusafirisha mizigo ndani na nje ya nchi na ni maalumu kwa ajili ya kubeba
mizigo tu ambapo kila moja ina uwezo wa kubeba mizigo yenye ukubwa wa tani elfu
moja na kila moja imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 5.5.
Aidha, Mhandisi
Nditiye amemuomba Mhandisi Khalid Songoro wa Kampuni ya Songoro Marine
Transport Boatyard ambao ni wakandarasi wanaojenga meli mpya ya abiria na
mizigo, kukarabati boti ya Jeshi la Polisi ya Mkoa wa Mbeya kwa gharama zao na
kufanya tathmini ya gharama inayohitajika kufanyia matengenezo meli ya MV
Songea iliyopo bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya ili iweze kutoa
huduma za usafiri.
Naye Mhandisi Songoro
ameridhia ombi la Mhandisi Nditiye, na kampuni yao itakarabati boti hiyo ya
Jeshi la Polisi, Mbeya pasipo wao kulipa gharama yoyote na kuwasilisha tathmini
ya matengenezo ya meli nyingine na kuwasilisha Wizarani.
Imetolewa
na kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 Comments