Katibu Mkuu wa Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akisisitiza
jambo kwa wataalamu wa sekta ya afya wakati wa kongamano la ubunifu na
utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania lililofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa LAPF, Dodoma
Mtendaji Mkuu wa Mfuko
wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga, akiwasilisha mada kuhusu
umuhimu wa tiba mtandao nchini kwa wataalamu wa sekta ya afya (hawapo pichani)
wakati wa kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao
Tanzania ambalo limeandaliwa na UCSAF lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano
wa LAPF, Dodoma
Kaimu Mkurugenzi wa
TEHAMA, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Peter Phillip Mwasalyanda
(aliyeketi katikati), akisikiliza kwa makini kongamano la ubunifu na
utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania ambalo limeandaliwa na UCSAF
lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma
Wataalamu wa sekta ya
afya wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt.
Mpoki Ulisubisya (hayupo pichani) wakati wa kongamano la ubunifu na utekelezaji
wa huduma za tiba mtandao Tanzania ambalo limeandaliwa na UCSAF lililofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma
........
Serikali imejipanga
kutumia tiba mtandao kuboresha huduma za afya nchini kwenye hospitali zote za
ngazi ya taifa, rufaa na wilaya ili kuwawezesha wagonjwa waishio sehemu mbali
mbali nchini kupata huduma za afya kwa wakati na kwa ufanisi.
Hayo yameelezwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua kongamano la ubunifu na utekelezaji wa
huduma za tiba mtandao Tanzania lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo
la LAPF, Dodoma.
Dkt. Ulisubisya
amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha watendaji wakuu wa
hospitali za taifa nchini, madaktari bingwa wa sekta ya Afya, wakuu wa taasisi
zinazoshughulika na sekta ya Afya, Wizara ya TAMISEMI, Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano; taasisi nyingine za Serikali; sekta binafsi na wabia wa maendeleo
ili kujadiliana na kuwa na uelewa wa pamoja wa kufanikisha utekelezaji wa
huduma za tiba mtandao ili kuboresha huduma za afya nchini.
Amesema kuwa tiba
mtandao itawezesha na kuongeza ufanisi katika kufanya uchunguzi, utoaji wa tiba
na madawa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza na
yanayotokana na ajali za barabarani. “Hadi hivi sasa ni asilimia 37 tu ya
wagonjwa wa kifua kikuu ndio wanaotambulika na kupatiwa huduma na Wizara ya
Afya katika hospitali mbalimbali nchini.
Hivyo, tiba mtandao itawezesha
upatikanaji wa wagonjwa na ufikishaji wa huduma kwao kwa wagonjwa wengine
asilimia 63”, amefafanua Dkt. Ulisubisya.
Ameongeza kuwa tiba
mtandao itapunguza gharama za wagonjwa na wanaowahudumia kusafiri kufuata
madaktari. Aidha, amewataka wakuu hao wa taasisi kuwaruhusu wataalamu wao, wa Wizara
ya TAMISEMI na wa Wizara ya Afya, kushiriki mafunzo ya tiba mtandao ili
kuongeza ufanisi wao katika kuhudumia wagonjwa.
Amewataka wataalamu wa
afya na wakuu wa taasisi zinazohusika na masuala ya afya kununua vifaa tiba vya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) vyenye viwango na ubora
unaohitajika ili kuwezesha tiba mtandao na manunuzi hayo yazingatie na kufuata
ununuzi wa pamoja wa huduma na bidhaa za Serikali.
Vifaa vya kisasa vya TEHAMA
vinavyohusika na tiba mtandao vitawawezesha wataalamu kufanya uchunguzi kwa
mgonjwa, kupata majibu ya uhakika na kumpatia mgonjwa tiba inayostahili na ya
uhakika.
Aidha, amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote
(UCSAF), Eng. Ulanga, ambao ndio waanadaji na waratibu wa kongamano hilo,
kushirikiana na TTCL kuhakikisha kuwa tiba mtandao inapatikana katika hospitali
zote za rufaa na hospitali ambazo zina changamoto ya kijiografia ya kufikika
kwa urahisi.
Aidha, hadi hivi sasa huduma ya tiba mtandao inapatikana katika
hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Bagamoyo, KCMC-Moshi, Bugando-Mwanza na
Benjamin Mkapa, Dodoma.
Naye Eng. Ulanga
amesema kuwa UCSAF imeanzisha huduma ya tiba mtandao kwenye vituo 14 vya
majaribio. Aidha, imeainisha orodha ya vituo 279 ikiwa ni pamoja na hospitali
za taifa, rufaa na wilaya ambazo zitaunganishwa na kuwezeshwa kutoa huduma ya tiba
mtandao nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, Dar es Salaam Dkt. Julius Mwaiselage,
akiwa mmoja wa washiriki wa kongamano hilo amesema kuwa, tayari tulikuwa
tunatumia huduma ya tiba mtandao kwa wagonjwa wetu kwa kushirikiana na
hospitali nyingine zilizopo nchini India kwa kuwafanyia wagonjwa uchunguzi na
kuona kama kweli mgonjwa husika anahitaji kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu
zaidi.
“Uwepo wa huduma ya tiba mtandao kwenye hospitali zetu nchini,
itatuwezesha kufanya uchunguzi na kutoa tiba kwa wagonjwa waliopo mikoani hivyo
kuwapunguzia gharama wagonjwa za kuja Dar es Salaam na endapo watalazimika kuja
basi watakaa kwa muda mfupi ukilinganisha na hapo awali”, amesema Dkt.
Mwaiselage. Washiriki wengine wa kongamano hilo ni kutoka Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, Bugando, MOI, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kiwete, Mloganzila, Aga
Khan, Hospitali ya Rufaa Mbeya, NHIF, PATH na Shirika la Afya Duniani.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment