Wanakijiji wa Kijiji cha Mauno Wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakichota
maji baada ya kuzinduliwa rasmi kwa kisima cha maji kilichojengwa na
wafadhili kutoka nchini Uturuki kupitia Ubalozi wa nchi hiyo hapa
nchini.
Wanakijiji
wa Kijiji cha Mauno Wilayani Kondoa mkoani Dodoma wakichota maji baada
ya kuzinduliwa rasmi kwa kisima cha maji kilichojengwa na wafadhili
kutoka nchini Uturuki kupitia Ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini.
Mmoja
wa akina mama wa kijiji cha Mauno, Kata ya Bumbuta, Jimbo la Kondoa
Vijijini akiongea na vyombo vya habari kuhusu furaha yao baada ya kisima
cha maji kuzinduliwa hatua iliyowaondolea kero ya kutembea mwendo mrefu
kutafuta maji
Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, na Mbunge wa Jimbo la KOndoa Vijijini, Dkt. Ashatu Kijaji (wa
pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wafadhili wa mradi wa
kisima cha maji pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ya kijiji na
viongozi wa dini katika kijiji cha Mauno, wilayani Kondoa.
Wakazi wa kijiji cha Mauno wakiwa
wamemwangusha ng'ombe kwa ajili ya kupata kitoweo ikiwa ni namna ya
kujipongeza na kusherehekea baada ya kuzinduliwa kwa kisima cha maji
kilichojengwa na wafadhili kutoka nchini Uturuki.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Na Benny Mwaipaja, Kondoa
ZAIDI ya
wakazi elfu 16 wa vijiji vitatu vya Mauno, Makiranya na
Kinyasi-Majengo, katika Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma
wameondokana na adha ya kukosa maji baada ya kuzinduliwa kwa visima
viatu vya maji vilivyojengwa kwa msaada wa wahisani kutoka nchini
Uturuki kupitia ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini
Akizungumza
wakati wa hafla ya uzinduzi wa visima hivyo katika Kijiji cha Mauno,
Kata ya Bumbuta, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge
wa Jimbo la Kondoa Vijijini Dokta Ashatu Kijaji, amesema kuwa
kuzinduliwa kwa visima hivyo kunalifanya jimbo lake lifikishe visima 41
hatua ambayo amesema itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji katika
jimbo lake.
Dkt. Kijaji ameushukuru Ubalozi wa Uturuki kwa
kuratibu msaada huo wa zaidi ya Dola za Kimarekani elfu 36, sawa na
shilingi milioni 81, zilizotumika kuchimba visima hivyo pamoja na kuweka
miundombinu mingine zikiwemo jenereta zinazotumika kusukuma maji hayo
na kuwezesha upatikanaji wa maji hayo.
"Hivi
sasa ujenzi wa visima 15 kati ya 25 vinavyojengwa na Serikali kupitia
Wizara ya Maji unaendelea huku wahisani wakiwa wametujengea visima 36
hivyo kufikisha idadi ya visima 61 katika kipindi cha miaka miwili tu
tangu Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
aingie madarakani hali ambayo haijawahi kutokea na lengo letu ni
kuhakikisha kuwa vijiji vyote 84 vinapatiwa huduma ya maji ifikapo mwaka
2020" Alisisitiza Dkt. Kijaji
Diwani wa Kata ya
Bunbuta Bw. Bashiru Mtolo na mkazi mmoja wa kijiji hicho Bi. Khadija
Hussein wamesema kuwa tatizo la maji katika kijiji cha Mauno lilikuwa
kubwa na kuwalazimisha wanawake na watoto kwenda umbali mrefu kusaka
maji kwa ajili ya matumizi yao ya majumbani pamoja na kunywesha mifugo.
"Tunaushukuru
Ubalozi wa Uturuki kwa msaada wao huu mkubwa na Mbunge wetu kwa
ufuatiliaji wake wa karibu uliowezesha kupatikana kwa visima hivi na
vingine ambavyo vimesaidia kwa kiwango kikubwa kutatua kero ya maji na
tunaamini mpaka kufikia mwaka 2020, matatizo ya maji katika wilaya yetu
ya Kondoa litakuwa historia" alisema Diwani Mtolo.
Naye
Mwakilishi na Mwambata wa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini Sheikh
Muhammad Cicek ameeleza kuwa msaada wa Dola elfu 36 zilizotumika kujenga
miradi hiyo mitatu ya visima vya maji umetolewa na wahisani mbalimbali
wa Uturuki ikiwa ni kuenzi uhusiano wa muda mrefu kati ya Uturuki na
Tanzania.
Alisema kukamilika kwa miradi hiyo ya maji
kutasadia kuwawezesha akina mama na wananchi wa Kondoa kwa ujumla
kufanya shughuli nyingine za maendeleo badala ya kutumia muda mwingi
kutafuta maji ambayo hata hivyo hayakuwa safi wala salama.





0 Comments