Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jason Rweikiza (Mb) akiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Henry Mambo (kushoto) kwenda kushuhudia jengo la chuo Tawi la Tabora lililojengwa kwa jitihada za chuo kwa kutumia fedha za ndani.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Jason Rweikiza (Mb) kushuhudia jengo la Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Tabora (linaloonekana) lililojengwa kupitia mapato ya ndani ya chuo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akitoa ufafanuzi kuhusu ujenzi wa jengo la chuo Tawi Tabora kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ilipoitembelea Kampasi hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Kampasi hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jason Rweikiza (Mb) akitoa pongezi kwa Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kwa ujenzi wa jengo la chuo katika Kampasi ya Tabora.
Mkuu
wa Mkoa wa Tabora Mhe. Aggrey Mwanri akiishukuru Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa kukitembelea Chuo cha
Utumishi wa Umma Tawi la Tabora kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo
la chuo katika Kampasi ya Tabora.
Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imeipongeza Menejimenti ya Chuo cha
Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kwa utendaji mzuri na ujenzi wa jengo katika
tawi la Tabora ambalo litatumika kutoa mafunzo
ya kozi mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuendesha shughuli
za kiutawala za chuo kwa ajili ya maendeleo ya chuo.
Pongezi hizo
zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za
Mitaa
Mhe. Jason Rweikiza (Mb) kwa niaba ya Kamati wakati wa ziara ya kamati hiyo ya
kutembelea jengo lililojengwa katika kampasi ya Tabora ili kujiridhisha na
maendeleo ya ujenzi.
Mhe. Rweikiza amesema
chuo kinastahili pongezi za dhati kwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa hadi kufikia
hatua ya kuezeka kwa kutumia mapato ya ndani ya chuo.
Aidha, Mhe.
Rweikiza ameiomba Serikali kusaidia fedha za ukamilishaji wa ujenzi wa jengo hilo
lililopo Kampasi ya Tabora kwani kozi zinazotolewa na chuo hicho kwa watumishi
wa umma na wananchi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Akitoa ufafanuzi
kuhusu ujenzi katika Kampasi hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na
Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu)
Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amesema jengo lilipofikia ni kwa jitihada za chuo
chenyewe, hivyo wizara wamekaa na kukubaliana kuelekeza nguvu katika
ukamilishaji wa ujenzi wa jengo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Mkoa, Mkuu wa Mkoa
wa Tabora Mhe. Aggrey Mwanri amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ni chuo
ambacho kimeishi kwa sura ya jina lake lenyewe hususani kwa jitihada zake kubwa
za ujenzi wa jengo katika kampasi ya Tabora na kuongeza kuwa jitihada hizo
zinaonesha kuwa mkoa na uongozi wa chuo unao uwezo wa kufanya makubwa ili
kukiendeleza chuo cha Utumishi wa Umma.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma
Tanzania Dkt. Henry Mambo akijibu swali kuhusu mpango wa chuo kufungua tawi
makao makuu Dodoma, amesema kuwa chuo kina nyumba ambayo ni ndogo iliyopo mtaa
wa Tabora na mwakani kimepanga kuifanyia ukarabati ili kianze kutoa kozi za
muda mfupi.
Dkt. Mambo ameongeza kuwa, Chuo kimepewa eneo la ekari
moja ambalo halitoshi kwa ujenzi hivyo wameiomba Manispaa ya Dodoma kuwapatia
ekari kumi (10) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa chuo mjini Dodoma.
Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) tawi la
Tabora kipo katika eneo la ekari 15.3 ndani ya Manispaa ya Tabora. Menejimenti
ya Chuo kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkurugenzi
wa Manispaa ya Tabora ipo katika hatua za mwisho za kupata Hatimiliki.
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
TAREHE 18 MACHI, 2018
0 Comments