Kinyang’anyiro Tuzo Maarufu za AMVCA 2018 chaanza
Dar es Salaam - Machi 2018;Baada ya kimya cha muda, Africa Magic
ikishirikiana na MultiChoice, hatimaye wametangaza rasmi kuanza kwa
kinyang’anyiro cha moja ya tuzo maarufu duniani katika tasnia ya sanaa ya
filamu zijulikanazo kama Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCAs).
Tuzo hizo ambazo hufanyika kila mwaka zimekuwa
zikihusisha mamia ya washiriki kutoka kila kona ya bara la Afrika na zimekuwa
moja ya tuzo zilizojizolea umaarufu mkubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla
na limekuwa ni jukwaa muhimu la kutambua na kuenzi vipaji vya tasnia ya filamu katika
bara la Afrika.
AMVCAs zilibuniwa kuthamini na kutambua mchango wa
watengeneza filamu wa Kiafrika, waigizaji na wataalam katika mafanikio ya sekta
ya filamu na televisheni ya bara hili na kutokana na mafanikio ya tuzo tano
zilizopita, maandalizi ya tuzo za mwaka huu ambazo zinatarajiwa kuwa kubwa na
za kuvutia zaidi yameanza na muamko tayari umeshaanza kuonekana na ushindani
unatarajiwa kuwa mkubwa sana.
Mkurugenzi wa MultiChoice Tanzania Maharage Chande
amebainisha kuwa wasanii wa Tanzania sasa wanaweza kuanza kuwasilisha kazi zao
kwa ajili ya tuzo hizo na kazi hizo zitaendelea kupokelewa hadi tarehe 30
Aprili 2018.
“Baada ya mapumziko mafupi, tunayo furaha kutangaza
kwamba mwaka 2018 utakuwa na toleo la
mwaka wa sita mfululizo wa MultiChoice na Africa Magic kuandaa AMVCAs kwa
mafanikio na tunaendelea kujivunia mabadiliko yanayoonekana kwenye nyanja ya
filamu tangu Tuzo zilipoanzishwa. Uwekezaji wetu endelevu unaonesha dhamira
yetu katikakusaidia kuibua na kuthamini vipaji barani Afrika na tunaamini
kwamba toleo la 2018 la AMVCAs litaacha alama kubwa zaidi katika sekta ya
utayarishaji filamu ya Afrika kuliko matoleo matano yaliyopita” alisema
Maharage.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukishiriki katika tuzo hizi
na wasanii wetu wa filamu wamekuwa wakifanya vizuri, lakini mwaka huu tunataka
tufanye vizuri zaidi na tuwe washindi katika Makundi mbalimbali ya tuzo hizo
kwani uwezo tunao” alisema Maharage na kusisitiza kuwa siri kubwa ni
kuhakikisha watanzania kwanza wanawasilisha kazi zao kwa wingi wakati huu na
kisha wakati wa kupiga kura ukifika tuhakikishe tunapigia kura kazi zetu na
wasanii wetu.
Katika Msimu uliopita, Filamu
za Kitanzania ziliwika katika kundi la Filamu Bora kabisa Afrika Mashariki
ambapo “Aisha” ya Amil Shivji, “Naomba
Niseme” ya Staford Kihore, na “Homecoming” ya Seko Shamte zilichaguliwa
huku “Siri ya Mtungi” ikijitokeza kwenye
kundi la Filamu Bora za lugha ya Kiswahili
Tanzania ina rikodi nzuri kwenye
tuzo hizi kwani misimu iliyopita filamu ya Kitendawili ya Richard Mtambalike
ilinyakua tuzo ya filamu bora ya lugha ya Kiswahili wakati Elizabeth Michael
‘Lulu’ alivuma katika tuzo hizo katika filamu yake ya Mapenzi iliyoteuliwa kuwa
filamu bora kabisa Afrika Mashariki.
Tuzo hizi za AMVCAs zinahusisha watengeneza filamu katika
vipengele mbalimbali kuanzia uigizaji na uongozaji mpaka uandishi na
utengenezaji na mwaka huu, tuzo kadhaa katika vipengele mbalimbali zitatolewa
kuanzia kwenye uigizaji na uongozaji mpaka uandishi na utengenezaji. Vipengele
vingine vitahusisha: filamu fupi au video za kwenye mtandao, muziki, ubunifu wa
mavazi, sauti na mwanga kati ya vingi vingine. Kwa 2018 kuna vipengele 27 kwa
ujumla, ambapo 7 viko wazi kwa ajili ya kura za watazamaji na 20 vitaamuliwa na
jopo la majaji wenye uzoefu mkubwa katika tasnia ya filamu ulimwenguni.
Kuingia AMVCAs ni bure na tarehe ya kufungwa kwa maingizo
ni 30 Aprili 2018. Filamu au sinema zilizotayarishwa kwa ajili ya televisheni
au tamthiliya za kwenye televisheni ambazo ziliingizwa mwanzoni au kuteuliwa
kwa ajili ya tuzo, au kutuzwa zawadi katika shindano lingine la filamu na
televisheni zinaruhusiwa kuingizwa kwenye AMVCAs kama zinarushwa au kuoneshwa
katika kipindi cha kuanzia Oktoba, 2016 hadi Machi, 2018.
Maelekezo ya kushiriki:
HATUA YA 1
Prepare a 2 to 3 minute long showreel for your online
submission. /Andaa ufupisho wa filamu yako wenye muda wakati ya dakika 2 hadi 3
kwa ajili ya kuuwasilishakwa njia ya mtandao
HATUA YA 2
Ingia www.africamagic.tvna uende kwenye ukurasa wa kuwasilisha.
HATUA YA 3
Jaza fomu za uwasilishaji na upandishe video yako.
Namba ya kipekee ya utambulisho itatolewa kwa kila ingizo la mtandaoni
lililokamilika. Kisha kutegemea na eneo ulipo, tuma ingizo lake akionesha namba
zake za utambulisho.
Kwa maelezo zaidi juu ya mahitaji ya kujiunga na taratibu za
uwasilishaji, tafadhali ingia www.dstv.com

0 Comments