Random Posts

Serikali Yatoa Hati za Hakimiliki za Kimila 275 kwa Wananchi wa Msalala Wilayani Kahama

 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jason Rweikiza (Mb) akimkabidhi Bi. Sabina Migayo Hati ya Hakimiliki ya Kimila wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - UTUMISHI na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lunguya  wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa yenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi  inayotekelezwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
 Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakipunga mikono kuwasalimu wananchi wa kijiji cha Lunguya  wilayani Kahama wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi.
 Mratibu wa MKURABITA Bi. Seraphia Mgembe (katikati ya umati) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lunguya wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa yenye lengo la kukagua maendeleo ya mradi ya MKURABITA.
 Baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Lunguya  wilayani Kahama wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jason Rweikiza (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua maendeleo ya miradi.
Mmoja wa wanufaika wa Hati ya Hakimiliki ya Kimila wilayani Kahama akitoa shukrani kwa Serikali kwa kitendo cha kutoa Hati za Hakimiliki za Kimila 275 kwa wananchi wa vijiji vya Lunguya na Segese.


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SERIKALI YATOA HATI ZA HAKIMILIKI ZA KIMILA 275 KWA WANANCHI WA MSALALA WILAYANI KAHAMA

Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) mkoani Shinyanga imepima mashamba 2158 na kutoa Hati za Hakimiliki za Kimila 275 kwa wananchi wa vijiji vya Lunguya na Segese wilayani Msalala.

Takwimu hizo za urasimishaji zimetolewa Bw.Leonard M. Mabula kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halimashauri ya Wilaya ya Msalala Bw. Simon Berege.

Akikabidhi Hati za Hakimiliki za Kimila kwa baadhi ya wananchi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Jason Rweikiza (Mb) amewata wananchi hao kuzitumia vizuri hati hizo ili waweze kujiondoa katika umasikini, kuboresha familia zao na wilaya yao.

Miongoni mwa wananchi waliopata fursa ya kukabidhiwa hati na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ni Bw. Kimbuya Shija, Bw. Daudi Steven Ntowe, Bw. Christopher Malajo, Bw. James Shija na Bi. Sabina Migayo.

Akizungumza na wananchi katika kijiji cha Lunguya, Waziri mwenye dhamana ya usimazi wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) nchini wa Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amesema Serikali inarasimisha ardhi za wananchi wa vijijini kuwa mali na kutoa hati za kimila zinazotambulika kwa mujibu wa sheria kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi wananchi wake.

Kapteni (Mstaafu)  Mhe. Mkuchika, amewahikishia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ina dhamira ya dhati ya kuboresha maisha ya wananchi wenye kipato cha chini kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA).

Naye, Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bi. Seraphia Mgembe amewata wananchi kutumia hati za kimila kupata mitaji, ameongeza kuwa Serikali inatoa hati hizo ili kuwawezesha wananchi wapate maendeleo kwa kutumia fursa hiyo kupata mitaji kutoka katika taasisi za kifedha.

Akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab R. Telack amefafanua kuwa, mradi umetekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya  Msalala katika vijiji viwili (2) vya Lunguya na Segese vilivyokuwa katika Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ambapo jumla ya hati za kimila 275 zimetolewa na MKURABITA.

Aidha, urasimishaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kama ilivyo katika Halmashauri nyingine nchini, umetoa matokeo chanya kwa kupunguza migogoro ya ardhi   iliyokuwepo na  kuongeza usalama wa milki za ardhi za wakulima waliorasimisha ardhi zao.

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS (UTUMISHI)
 TAREHE 16 MACHI, 2018

Post a Comment

0 Comments