Dkt. dhamana wa meno kanda ya Unguja Muhidini Abdalla
akiwapatia elimu fupi wanafunzi wa skuli ya Mwanakwerekwe E namna ya
kusafisha meno.
Mwanafunzi Ali Makame wa skuli ya Mwanakwereke E akiwaonesha
mfano wa kusafisha meno wanafunzi wezake baada ya kupatiwa elimu ya
usafishaji wa meno skulini hapo.
Dkt. bingwa wa meno kutoka Chuo kikuu cha AJMANI cha Falme za
kiaarabu Zaid Mohammed Hassan akimfanyia uchunguzi wa meno mwanafunzi
wa skuli ya Mwanakwerekwe H Juma Hassan katika zoezi la kutoa matibabu
yaliofanyika skulini hapo.
Dkt bingwa kutoka Ujerumani Isabella Di Lorenzo akimfanyia
uchunguzi wa meno mwanafunzi wa skuli ya Mwanakwerekwe H Raiyani Subeti
Mkaazi wa Magomeni katika matibabu yaliofanyika skulini hapo.
Daktari dhamana wa Meno kanda ya Unguja alievalia vazi jeupe
Muhidini Abdalla akishirikiana na madaktari bingwa kutoka Ujerumani na
Falme za Kiarabu wakimng’oa jino mwanafunzi Aisha Makame wa skuli ya
Mwanakwerekwe H katika matibabu yaliofanyika skulini hapo.
Mwalimu Mkuu wa skuli ya
Mwanakwerekwe E Khityar Haidhuru Ramadhan akizungumza na waadishi wa
habari kuhusuana na zoezi hilo na kuishukuru Wizara ya Afya Zanzibar kwa
kuwapatia matibabu wanafunzi wa skuli hizo.
Picha na Abdalla Omar Habari Maelezo
Na Kijakazi Abdalla-MAELEZO
JAMII imetakiwa itumie mbinu sahihi ili kuimarisha afya kinywa na meno na kupunguza mzigo mkubwa wa kutibu maradhi ya meno.
Akizungumza katika kampeni maalum
juu ya kujikinga na maradhi yanayoathiri kinywa na meno katika skuli ya
msingi Mwanakwerekwe ‘E’, Daktari Dhamana Kanda ya Unguja Muhidin
Abdalla Mohammed, amesema wananchi wengi wamebainika kuathiriwa na
maradhi ya kinywa na meno.
Kwa hivyo amesema ipo haja ya kuchukua tahadhari ili kupunguza tatizo hilo.
Aidha, alisema lengo la kampeni
hiyo ni kuinua uwelewa wa watu ambao hawatoi kipaumbele kwa afya ya
kinywa na meno, na hivyo kujikuta wakisumbuka kuhahangaikia matibabu.
Dk. Muhiddin pia amesema hatua ya
kufanya kampeni hiyo katika skuli, inalenga kuwapa elimu wanafunzi juu
ya namna bora na sahihi za kutunza meno na kupiga mswaki ili waimarishe
afya ya meno yao.
Alisema katika umri mdogo, ndipo
watoto hupitia mabadiliko makubwa kimwili, hivyo kuwapa taaluma
kutawawezesha kufahamu mbinu sahihi za kuimarisha afya na kujikinga
wanapokua wakubwa.
Hata hivyo, ameiomba Serikali
iongeze juhudi zaidi kufikisha huduma za meno kila eneo ingawa
kunahitaji gharama kubwa, lakini akasema kuacha watu waugue bila tiba ni
gharama zaidi.
Alieleza kuwa, tangu kuanza
kampeni hizo kuelekea maadhimisho ya siku ya afya ya kinywa na meno
kimataifa, zaidi ya watoto 1,000 wametibiwa kwa kushirikiana na
madaktari kutoka Ujerumani, Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) pamoja na
Wizara ya Afya.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi
Mwanakwerekwe ‘E’ Khitiyar Haidhuru Ramadhani, alisema ujio wa
madaktari hao umewapa faraja wanafunzi na elimu sahihi ya kutunza meno
yao.
Aidha aliwataka wazee kujenga
utamaduni wa kuwanunulia watoto vitu vinavyoweza kuwaepusha na maradhi
ya meno kama vile pipi, biskuti na chokoleti ambavyo huchangia zaidi
maradhi hayo.
Mwalimu huyo pia aliwaomba wazazi
kuwasimamia vyema watoto na kuhakikisha wanapiga miswaki mara mbili kwa
siku na kwa njia sahihi kwani imebainika kuna baadhi ya wanafunzi huenda
skuli bila kusafisha meno yao.
Aidha aliiomba Wizara ya Afya
iliendeleze zoezi la kuchunguza maradhi yote kwa wanafunzi, kwani
kumekuwa na ongezeko kubwa la maradhi lakini baadhi ya wazee hawamudu
gharama za uchunguzi na tiba.






0 Comments