Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akifafanua jambo kwa
waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ziara yake kwa taasisi za
mawasiliano Zanzibar. Kushoto ni Kaimu Posta Masta Mkuu wa Shirika hilo Bwana
Hassan Mwang’ombe na kulia ni Mkurugenzi wa Huduma wa Shirika la Simu Tanzania
(TTCL) Bwana Hussein Selemani Nguvu.
Naibu Waziri wa
Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameupa Mfuko wa Mawasiliano
kwa Wote (UCSAF) wiki mbili kwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano ya simu za
mkononi na kuwasilisha taarifa hiyo ofisini kwake.
Mhandisi Nditiye
ameyasema hayo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi Zanzibar ya kukagua hali ya
mawasiliano kisiwani humo na kutembelea taasisi za mawasiliano zilizo chini ya
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambapo suala la mawasiliano ni la
muungano.
Nditiye amesema kuwa
amepokea taarifa kutoka kwa wabunge wa Kisiwa cha Zanzibar kuwa hali ya
mawasiliano kwenye kisiwa hicho sio nzuri na sehemu nyingine hakuna mawasiliano
licha ya kuwa kuna minara ambayo inatoa huduma za mawasiliano ila kutokana na
jiografia ya Pemba ambapo kuna milima na mabonde hivyo mawasiliano si ya
uhakika.
“Nawaagiza muende Pemba mkaainishe maeneo yote ambayo hayana
mawasiliano na muwasilishe taarifa hiyo ofisini kwangu baada ya wiki mbili,”
amesema Mhandisi Nditiye.
Meneja wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) Ofisi ya Zanzibar Bi. Esuvatie-Aisa Masinga wakati
akiwasilisha taarifa yake kwa Mhandisi Nditiye kuhusu majukumu ya ofisi yake ya
usimamimizi na udhibiti wa mawasiliano na posta, amekiri kuwa yapo baadhi ya
maeneo Pemba na Unguja ambapo hali ya mawasiliano sio nzuri na hairidhishi.
Ameongeza kuwa Pemba
kuna maeneo ambayo hakuna mtoa huduma na pale ambapo mawasiliano yapo bado
ubora wa huduma sio nzuri. Pia ameyataja maeneo yasiyo na mawasiliano kwa
upande wa Mkoani kuwa ni Kengeja na Chokochoko na kwa upande wa Micheweni ni
Konde na Gando.
Amefafanua kuwa sehemu
nyingine za Pemba mtandao wa Zantel upo lakini ‘coverage yake’ sio nzuri.
“Ili
kufanya mawasiliano yawe mazuri kwa Pemba, ni muhimu ‘site’ zikaongezwa hasa
ukizingatia hali ya kijiografia ya kisiwa hicho,” amesema Masinga.
Mawasiliano
ya kisiwa cha Pemba hayaridhishi, tunapendekeza Serikali kupitia UCSAF kuweka
minara zile sehemu ambazo hakuna mawasiliano.
Naye mwakilishi wa
UCSAF Bwana John Munkondya amepokea maelekezo ya Mhandisi Nditiye ambapo Mfuko
huo utakwenda Pemba kukagua hali ya mawasiliano na kuwasilisha ripoti ofisini
kwake ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata mawasiliano ya uhakika.
“Sisi
kama UCSAF tumechukua taarifa hii ya maeneo ambayo hayana mawasiliano,
tutakwenda Pemba kukagua na maeneo hayo yataingizwa kwenye utaratibu wa kanda
maalumu ili tuweze kufikisha mawasiliano,”amesema Munkondya.
Katika hatua nyingine,
Mhandisi Nditiye amekagua utendaji kazi wa moja ya scanner mpya ambazo Wizara
yake imeipatia Shirika la Posta Tanzania ili ziweze kutumika kukagua mizigo, vifurushi na vipeto ambavyo
vinaingia na kutoka ndani na nje ya nchi ili kudhibiti uingizaji na
usafirishaji wa bidhaa na vifaa ambavyo ni hatarishi kwa usalama wa raia na
taifa letu.
Kaimu Posta Masta Mkuu
wa Shirika la Posta Tanzania Bwana Hassan Mwang’ombe amemweleza Mhandisi
Nditiye kuwa Wizara yake imewapatia scanner
nne zenye thamani ya shilingi milioni 421 ambapo tayari zimefungwa kwenye mikoa
mbali mbali ili ziweze kuwasaidia kupunguza udanganyifu ambao unajitokeza
ambapo baadhi ya wateja wasio waaminifu wamekuwa wakisafirisha baadhi ya vifaa
na bidhaa kama vile madawa ya kulevya kinyume na sheria za nchi.
Pia, Mhandisi Nditiye
ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi, ufungaji wa samani na uwekaji wa
vifaa vya TEHAMA kwenye moja ya kituo cha mawasiliano kilichojengwa na UCSAF
kwa lengo la kuwapatia wananchi huduma za mawasiliano.
Munkondya amemweleza
Mhandisi Nditiye kuwa UCSAF imejenga vituo kumi vya mawasiliano kwa gharama ya
shilingi milioni 721 na ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98 ambapo vituo
sita vipo Unguja na vine vipo Pemba.
Ameongeza
kuwa UCSAF inaweka samani, vifaa vya TEHAMA pamoja na kompyuta kumi kwa kila
kituo, kujenga choo na uzio ili wananchi waweze kupata huduma ya mawasiliano
kwa gharama nafuu.
Naye mjumbe wa Bodi ya
TPC Bi. Khadija Shaban amemuomba Mhandisi Nditiye kuwa vituo hivyo vya
mawasiliano vya Pemba na Unguja visimamiwe na kuendeshwa na TPC ili viweze kudumu
kwa muda mrefu kama ambavyo inafanyika hivyo Tanzania Bara.
Mhandisi Nditiye akiwa
katika ziara yake kisiwani Unguja, ametembelea na kukagua mitambo ya Shirika la
TTCL, hali ya biashara na namna wanavyowahudumia wateja ambapo ameona
miundombinu ya Shirika hilo inavyosambaza huduma za mawasiliano kutoka Tanzania
Bara kuja kisiwa cha Zanzibar.
Nditiye ameiagiza TTCL
kufunga mitambo ya mawasiliano kwenye meli za maziwa makuu na baharini ili
wananchi wanaposafiri waweze kupata mawasiliano ya uhakika ya simu za mkononi
na huduma za intaneti.
Pia, ameiagiza TCRA
kuwasajili watu wote wanaosafirisha mizigo, vifurushi na vipeto na kuwapatia
leseni ili walipe gharama ya kufanya huduma hiyo ili wananchi wawatambue na
kuwa na imani nao hasa pale ambapo mzigo unapotea waweze kulipwa na Serikali
iweze kupata mapato yake.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 Comments