Meneja wa mamlaka ya mawasiliano Kanda ya Mashariki (TCRA) ,Injinia Anneth Matindi akizungumza kuhusiana na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki ya watumiaji ,katika chuo cha sanaa na utamaduni Bagamoyo (TASUBA) ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni kuwezesha soko la mtandaoni kwa haki.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Mgeni rasmi ambae ni mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, alhaj Majid Mwanga akiongea juu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki ya watumiaji ,katika chuo cha sanaa na utamaduni Bagamoyo (TASUBA) ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni kuwezesha soko la mtandaoni kwa haki(picha na Mwamvua Mwinyi)
Wanachuo wa chuo cha taasisi ya sanaa na utamaduni Bagamoyo (TASUBA) wakisikiliza kwa makini mada mbalimbali zilizotolewa kuhusiana na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki ya watumiaji ,katika ukumbi wa chuo hicho ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni kuwezesha soko la mtandaoni kwa haki
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WATUMIAJI wa mawasiliano katika teknolojia ya kidigital nchini Tanzania ,wameongezeka kutoka mil.3.5 kwa mwaka 2008 hadi kufikia mil.23 mwezi Desemba mwaka 2017 .
Aidha kwa dunia ,watumiaji wameongezeka kutoka asilimia moja kwa mwaka 1995 na kufikia asilimia 50 mwaka uliopita.
Meneja wa mamlaka ya mawasiliano Kanda ya Mashariki (TCRA) ,Injinia Anneth Matindi alieleza hayo, katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki ya watumiaji ,yaliyofanyika chuo cha sanaa na utamaduni Bagamoyo (TASUBA) ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni kuwezesha soko la mtandaoni kwa haki.
Alisema, teknolojia ya kidigital katika mawasiliano imeleta chachu na faida ndani ya jamii lakini pia ina athari kubwa endapo mtumiaji anatumia vibaya.
Injinia Anneth alisema kuwa ,mitandao imeweza kupanua wigo na kuinua biashara ya mtandao kwani watu wamekuwa wakinunua bidhaa mbalimbali kupitia mitandao hiyo.
"Kufanya biashara- E commerce watumiaji sasa wanaweza kununua ticket na bidhaa nyingi kwa kutumia mitandaoni ,biashara zimepanuka "
"Lakini licha ya faida zote bado kuna mambo yanayotakiwa kufanyiwa kazi kwani baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mitandao vibaya kwa kufanya uhalifu,uchochezi,kudhalilisha na na udanganyifu " alieleza Injinia Anneth.
Hata hivyo, injinia Anneth alielezea soko la mitandao liwe la haki na salama ili kuendelea kupata manufaa na kuinua soko ndani na kimataifa.
Nae mgeni rasmi ambae ni mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, alhaj Majid Mwanga alisema, waathirika wakubwa kwenye jamii ni wanachuo ambao wapo waliopata kesi kutokana na kutumia vibaya mitandao na kujikuta wakiishia jela.
"Wengine hawajui kabisa matumizi ya mtandao ,wanafuata mkumbo,wanashindwa kutumia mitandao ili kuinua taaluma zao ,wanagoole mitandao ya ngono na mengine isiyo na tija kwao" alisisitiza alhaj Mwanga.
Alhaj Mwanga aliwataka wanachuo hao kuwa mabalozi kwa wasanii na vijana wenzao ili hali kuondoa kero zinazojitokeza.
Mkuu huyo wa wilaya ,aliitaka TCRA kwenda kusimamia baadhi ya vyombo vya habari (Tvs na Radio)ambavyo bado watangazaji wake wanatoa mambo ambayo jamii haipaswi kusikiliza wala kuona.
"Mkaangalie pia haya makampuni ya simu ambayo yanaweka miziki kiholela bila mlaji /mteja kuomba ambapo wamekuwa wakitukata makato yasiyo ya ridhaa yetu ,unakuta wanamwekea mteja muitiko wa wimbo mwanaume machine wakati mtumiaji ni sheikh, kiongozi mkubwa ," alisema alhaj Mwanga.
Awali akitoa mada ya matumizi bora ya mtandao, injinia Christopher John kutoka TCRA Kanda ya Mashariki, aliitaka jamii kuepuka tabia ya kutoa namba za siri za simu kwa mtu wanaedhani wanamuamini.
Alisema wahakikishe wanafanya matumizi salama na sahihi ya huduma za mawasiliano kwa manufaa ya kila mmoja ili kujiepusha kuingia matatani bila sababu ya msingi.
'"Msirushiane taarifa zisizo za uhakika katika makundi ya kijamii au kwa wenzako ",taarifa za aina hiyo zitakuletea madhara, na kukuingiza matatani hivyo jaribuni kujiepusha na matumizi mabaya ya mawasiliano,"; ukipatwa na tatizo piga mawasiliano TCRA
0222412011,0784558271-70" alisema Injinia John.
Mtendaji mkuu wa taasisi ya Sanaa na utamaduni (TASUBA), dk.Herbert Makoye na rais wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo ,Isdory Moshi ,walishukuru kwa mafunzo na elimu waliyopatiwa wanachuo .
Walisema wanachuo wengi huwa wakijikita kwenye matumizi yasiyo sahihi ya mtandao hasa ya kijamii ,hivyo watakuwa mabalozi wa kukemea mabaya kwa wengine.



0 Comments