TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
WIZARA
SABA KUKUTANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAZINGIRA YA BIASHARA NA UWEKEZAJI MPAKANI
MWA TANZANIA NA ZAMBIA
Ofisi ya
Waziri Mkuu chini ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
Nchini, imeamua kuzikutanisha wizara saba zinazohusika moja kwa moja na
changamoto zinazopunguza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara na
Wawekezaji mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Akiongea
wakati wa ziara ya kutembelea maeneo ya utekelezaji wa Mpango wa maboresho ya
Mazingira ya biashara na uwekezaji katika mkoa wa Songwe na maeneo yaliyopo
mpakani mwa Tanzania na Zambia, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na
Uratibu), Profesa, Faustin Kamuzora amesema mara baada ya kuhitimisha ziara yake
tarehe 17 Machi, 2018, atakutana na makatibu wakuu wa wizara zinazopaswa
kutoa suluhisho la changamoto hizo.
“Nitakutana na makatibu wakuu wenzangu kutoka
Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya nje na Ushrikiano
wa Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za
mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) na
naamini maazimio tutakayotoa katika kikao hicho yatakuwa suluhisho la kuondoa
changamoto zinazojitokeza hapa mpakani mwa Tanzania na Zambia” , amesema
Kamuzora.
Akibainisha
changamoto za mazingira ya Biashara na uwekezaji mpakani mwa Tanzania na
Zambia, Mkuu wa mkoa wa Songwe, Luteni Mstaafu, Chiku Galawa amesema,
changamoto kubwa mpakani hapo ni usalama kwa wafanyabiashara na biashara zao,
ambapo kwa mazingira ya mpaka huo imekuwa vigumu kuuimarisha.
“Mpaka wetu umejengwa kila mahali , hivyo uhalifu
unakuwa mgumu kuuzuia Kuna watu wanakunywa pombe Zambia ambazo tumezizuia hapa
nchini kuuzwa, na kurudi wamelewa Tunduma, suala la biashara haramu ya ubadilishaji
wa fedha inayofanywa mtaani kinyume na
sheria na taratibu za nchi ni changamoto , lakini wafanyabiashara wanakwepa
kodi kutokana na kuwa kunabaadhi ya watanzania sehemu ya nyumba zao zipo Zambia nyingine ipo Tanzania hivyo ushuru
wa forodha haukusanywi kwa madai wanapeleka bidhaa hizo kwa watanzania kwani
hawapitishi bidhaa hizokwenye lango husika” alisema Galawa
Galawa
amebainisha mipango ambayo Mkoa umejipanga katika kuhakikisha wanakabili
changamoto hizo, kuwa ni kuliweka Daftari la wakaazi katika mfumo wa
kielektroniki ambalo litajumuisha wakaazi wote wa Tunduma kuanzia umri wa mwezi
mmoja na litakuwa linahuishwa kila wakati, Upimaji wa mji waTunduma nao
unaendelea na kila mmiliki wa ardhi
atapewa hati, pia litajengwa soko kubwa mpakani hapo ili kufanya menejimenti ya
biashara mpakani.
Aidha,
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu alikutana na wadau wa sekta binafsi, pamoja na
wateja katika Kituo cha Forodha cha Pamoja Tunduma, ambao walishauri sekta
zinazohusika na Mazingira ya Biashara na Uwekezaji mpakani hapo kwa upande wa
Tanzania na Zambia zikutane ili kuharakisha kutatua changamoto zinazopunguza
ufanisi wa biashara mpakani hapo.
Lengo la Mpango
wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini ni Kupunguza gharama za
Kufanya biashara nchini kwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa
wafanyabiashara na Wawekezaji, mpango huo unaotekelezwa na Idara, Wizara na
Wakala wa Serikali kwa uratibu wa Ofisi
ya Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA
MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI
YA WAZIRI MKUU
|
0 Comments