Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
................................................................................
Serikali imeahidi kuboresha
miundombinu na fursa nyingi za kiuchumi
katika maeneo ya vijijini ili kuweka mazingira bora na salama
yatakayovutia wawekezaji katika sekta
mbalimbali hususani Sekta ya Fedha.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma
na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kalenga (CCM) Mhe. Godfrey Mgimwa
aliyetaka kujua tamko la Serikali juu ya idadi kubwa ya benki za biashara
kufunguliwa kwenye miji mikubwa.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji
alisema kuwa miji mikubwa inakidhi
vigezo muhimu vya uwekezaji kwa Sekta ya Fedha kama vile uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi,
miundombinu ya kisasa na usalama ikilinganishwa na maeneo ya vijijini.
Alisema kuwa kufuatia mabadiliko ya
mfumo wa kiuchumi nchini unaotekelezwa tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990,
shughuli nyingi za kiuchumi hususani benki zinaendeshwa na Sekta Binafsi .
“Kwakuwa Sekta Binafsi lengo lake ni
kufanya biashara na kupata faida, uwanzishaji wa huduma za kibenki hutegemea
upembuzi yakinifu ambao unazingatia fursa za kiuchumi zilizopo katika eneo
husika, uwepo wa miundombinu wezeshi na usalama”, alisema Dkt. Kijaji.
Alifafanua kuwa Serikali inachokifanya
ni kuweka mazingira bora yatakayowavutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza
maeneo ya vijijini kwa kuwa lengo ni kufikisha
huduma za kifedha kwa watanzania wote.
Katika swali la nyongeza la Mbunge
huyo, alitaka kujua mbinu mbadala ya Serikali kuhakikisha inapeleka huduma za
benki vijijini, kwa kuwa mpaka sasa Serikali bado haijaunda Sera ya kuhakikisha
huduma hizo zinawafikia walengwa hasa wa vijijini.
Dkt. Kijaji alieleza kuwa mpango
mbadala wa kuhakikisha huduma za kibenki zinafika vijijini upo na Serikali inausimamia
vizuri, na kuongeza kuwa mpango huo umeiwezesha Tanzania kuongoza katika huduma
za fedha jumuishi barani Afrika.
Aidha Dkt. Kijaji alifafanua kuwa uwepo wa mawakala wa
benki, kutolewa kwa huduma za kibenki kupitia Kampuni za simu ni ishara tosha
kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi
wote.
0 Comments