MSHAMBULIAJI
wa Lipuli ya Iringa, Adam Salamba amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa
mwezi Machi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL)Tanzania Bara.
Salamba
alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Salum
Kimenya wa Prisons na kipa wa Azam, Mwadini Ally katika uchambuzi uliofanywa
wiki hii na Kamati ya Tuzo hizo.
Mshambuliaji
huyo kwa Machi alionesha uwezo mkubwa na kuisaidia timu yake kupata mafanikio
akifunga mabao matatu kwa dakika 270 alizocheza, ambapo Lipuli ilicheza michezo
mitatu ikishinda miwili na kutoka sare mmoja na kupanda kwa nafasi moja kutoka
ya nane hadi ya saba kwa mwezi huo.
Kwa
upande wa Kimenya alicheza dakika 269 na kufunga mabao mawili, akiiwezesha
Prisons kushinda michezo miwili kati ya mitatu iliyocheza na kutoka sare mmoja,
ikipanda kutoka nafasi ya tano hadi ya nne.
Mwadini
yeye alicheza dakika zote 270 ambazo timu yake ilicheza kwa mwezi Machi,
ikishinda michezo yote mitatu iliyocheza, ikibaki katika nafasi yake ya tatu.
Kutokana
na ushindi huo, Salamba atazawadiwa tuzo, kisimbusi cha Azam na fedha taslimu
sh. Mil. Moja kutoka kwa wadhamini Vodacom.
Wachezaji
wengine ambao tayari wameshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi wa VPL msimu huu
na miezi yao katika mabano ni mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (Agosti),
beki wa Singida United, Shafiq Batambuze (Septemba) na mshambuliaji wa Yanga,
Obrey Chirwa (Oktoba).
Wengine
ni kiungo wa Singida United, Mudathir Yahya (Novemba), mshambuliaji wa Mbao FC
ya Mwanza, Habibu Kiyombo (Desemba), mshambuliaji wa Simba, John Bocco
(Januari) na kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi (Februari).
Tuzo za
Mchezo Bora wa jumla wa Ligi Kuu Tanzania Bara zinatarajiwa kufanyika baadaye
mwaka huu katika tarehe itakayotangazwa, ambapo licha ya Mchezaji Bora, pia
kutakuwa na tuzo nyingine tofauti kwa kategori mbalimbali.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA
MIGUU TANZANIA TFF

0 Comments