Random Posts

Balozi Seif Akutana na Kufanya Mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya Kifalme ya Oman

 Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya  Kifalme ya Oman Bwana Salum Mohamed Al-Mahrooqi kulia aliyevaa kilemba akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
.Bwana Salum Mohamed Al- Mahrooqi aliyenyanyua Mkono akielezea mikakati ya Oman katika kuendeleza Uhusiano na Zanzibar wakati akizungumza na Balozi Seif Ali Iddi wa kwanza kutoka Kulia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa kwanza Kutoka Kulia akiishukuru Serikali ya Oman kwa misaada inayoendelea kutoa kwa Zanzibar.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya  Kifalme ya Oman Bwana Salum Mohamed Al- Mahrooqi aliyevaa Kilemba akifafanua jambo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao na Balozi Seif.

Kushoto ya Bwana Salum Mohamed Al-Mahrooqi ni Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo na kulia ya Balozi Seif ni Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed.
.......................................................

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya  Kifalme ya Oman Bwana Salum Mohamed Al-Mahrooqi alisema uwepo wa Jumla la Ajabu liliopo Forodhani Mji Mkongwe maarufu 'Beit Al Ajaib' utaendelea kuwa utambulisho wa Zanzibar Kimataifa katika masuala ya Kihistoria na Utamaduni.


Alisema Jengo hilo Maarufu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Dunia tokea Karne ya 17 linastahiki kufanyiwa ukarabati makubwa ili kulirejeshea hadhi yake ya kawaida na Oman tayari imeahidi kugharamia ukarabati hayo.

Bwana Salum Mohamed Al-Mahrooqi aliyeambatana na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ahmad Hamoud Al Habsy alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katibu Mkuu Salum alisema hatua ya Serikali ya Oman kuahidi kutoa gharama za ukarabati ya Jumba hilo imekuja kutokana na Historia kubwa ya Uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Oman kwa Karne kadhaa zilizopita.

Alisema Historia ya pande hizo mbili zenye udugu wa Damu hasa katika masuala ya Utamaduni utaendelea kuwepo na kuimarishwa kwa faida ya Vizazi vya sasa na vile vitakavyokuja  hapo baadae.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mambo ya Kale wa Oman alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ziara ya  Ujumbe wake  Visiwani Zanzibar umekusudia kufanya uratibu wa ushirikiano wa mambo kadhaa yatakayowezesha kusaidia na kuimarisha ushirikiano wa pande hizo mbili.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar  bado ni tulivu na kuwaomba Waoman  kutumia fursa iliyopo ya Zanzibar ni Njema kufika kujifunza mambo tofauti ya Kihistoria ambayo yana mafungamano ya Oman.

Balozi Seif aliuhakikishia Ujumbe huo wa Oman  kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano kwa ndugu zao wa Oman na kusema kwamba, wasimamizi pamoja na wajenzi wa ukarabati huo wa Jumba la Beit Al Ajaib watepewa msaada wa kina katika kuona kazi hiyo inafanyika na kumalizika kwa mafanikio makubwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwa kutoa mfano, kwamba mambo yaliyopo Zanzibar yenye mafungamano na uhusiano na Oman ni Majengo ya Kihistoria yaliyopo Mji Mkongwe ambayo yataendelea kutunzwa ili yabaki kuwa kumbukumbu nzuri ya kukuza ushirikiano wa pande hizo mbili.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mambo ya Kale wa Oman Bwana Salum Mohamed Al- Mahrooqi na Ujumbe walitembelea sehemu mbali mbali za Kihistoria, maeneo ya mashamba ya Viungo pamoja na kukutana na Viongozi mbali mbali wanaohusika na masuala ya Mambo ya Kale.

Picha na habari Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa Kushirikiana na
Idara ya Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika Mashariki Ofisi ya Zanzibar

Post a Comment

0 Comments