Subscribe Us

header ads

Balozi Seif Akutana na Kufanya Mazungumzo na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CCECC ya China

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akisalimiana na Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya Civil Engineering Construction Corporation 'CCECC' ya China Bw. Zuang Shangbiao Vuga Mjini Zanzibar.
 Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CCECC ya China Bw. Zuang Shangbiao wa tatu kutoka Kulia akielezea shukrani zake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kwa kuiamini Kampuni yake kujenga Bara bara ya Bububu hadi Mkokotoni kupitia Mahonda na Kinyasini Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mhe.  Mohamed Aboud Mohamed.

 Balozi Seif kushoto akisifu umahiri wa Kampuni za Kichina zinazofanya kazi Nchini Tanzania wakati akibadilishana mawazo na Rais wa Kampuni ya CCECC Bw. Zhuang Shangbiao aliyekaa upande wa Kushoto.
 Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya CCECC ya China Bw. Zuang Shangbiao Kushoto akimkabidhi zawadi ya picha ya Ukuta Mkuu wa China 'Great Wall' Balozi Seif mara baada ya mazungumzo yao.
Bwana Zuang Shangbiao Kushoto akifurahia zawadi ya  viungo aliyokabidhiwa na Balozi Seif baada ya mazungumzo yao.
........................................................
Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya Nchini China ya Civil Engineering Construction Corporation 'CCECC' Bw. Zhuang  Shangbiao alisema hatua iliyochukua  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  'SMZ' ya kuipa kazi ya ujenzi wa barabara Nchini imeleta heshima kubwa na ya kipekee kwa Kampuni hiyo.

Alisema kazi iliyo mbele kwa uongozi na wahandisi wa kampuni hiyo hivi sasa ni kujipanga vyema katika kuhakikisha heshima waliyopewa na SMZ wanailinda
katika kuwajibika ipasavyo  wakati wa utekelezaji wa jukumu hilo zito katika misingi ya ari na bidii kubwa.

Bwana Zhuang  Shangbiao akiuongoza Ujumbe wa Viongozi saba wa Taasisi hiyo ya Civil Engineering Construction Corporation alisema hayo wakati akitoa
shukrani katika mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema uzowefu wa ujenzi iliyokuwa nayo Kampuni hiyo ya CCECC kwa zaidi ya Miaka 50 iliyopita inahamishiwa Zanzibar  katika ujenzi wa barabara
inayoanzia Bububu, Mahonda  kupitia  Kinyasini hadi Mkokotoni yenye urefu
wa Kilomita 31.

Bwana Zhuang alimthibitishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba
Wahandisi wa Ujenzi wa Kampuni ya CCECC watakamilisha kazi hiyo kwa wakati ulliopangwa na katika kiwango kinachokubalika Kimataifa kwa vile wana utaalamu na uzoefu wa kutosha.

Alifahamisha kwamba CCECC  ilishasaini mikataba ya kazi yenye thamani ya  zaidi ya Dola za Kimarekani Bilioni 240 duniani mwaka uliopita na hivi sasa kampuni hiyo inashikilia nafasi ya 58 kwa ubora kati ya 500 Duniani katika masuala ya jenzi wa miundombinu ya madaraja, barabara na mambo mengine.

Rais  huyo wa Kampuni ya CCECC alieleza kuwa uongozi wake ambao tayari
umeshafungua Matawi takriban katika  Mataifa 18 Duniani na Bara la Afrika
umelenga kusaidia huduma za Kijamii katika kuhakikisha uhusiano wake na Mataifa hayo unaendelea kudumu.

Alisema CCECC yenye utaalamu mkubwa iko tayari pia kuwekeza katika miradi
ya ujenzi wa Nyumba za Makaazi na biashara sambamba na kuitikia wito wa
uanzishaji wa Viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya uvuvi wa Bahari Kuu utakaotoa ajira pana zaidi kwa Vijana.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema Kampuni za Kichina zinastahiki kupongezwa  kutokana na bidii
kubwa ya Wahandisi wake katika ujenzi wa Miundombinu tofauti hapa Nchini.

Balozi Seif alisema takwimu zinaonyesha wazi kwamba hivi sasa Kampuni za
Kichina zinaongoza kwa kuaminiwa kupewa miradi mbali mbali ya Ujenzi katika
Taasisi tofauti za Umma na hata zile Binafsi.

“ Kampuni za Uhandisi wa Ujenzi ya Jamuhuri ya Watu wa China hazina tabia
ya kukimbia kazi zinazopewa tofauti na baadhi ya Kampuni nyengine za kigeni
zinazoingia mitini baada ya kushindwa kukamilisha kazi ”. Alisema Balozi
Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Rais huyo wa Kampuni ya CCECC kwamba kukamilika kwa Ujenzi wa Bara bara hiyo ya Bububu, Mahonda kupitia Kinyasini hadi Mkokotoni kutasaidia kuleta matumaini makubwa kwa Wananchi waliowengi.

Balozi Seif aliushauri na kuuomba uongozi wa Kampuni ya CCECC kuwa
mabalozi wa kuitangaza  Zanzibar zaidi kwa Makampuni mengine ya uwekezaji
ya Nchini China kufikiria kuwekeza miradi yao ya kiuchumi hata kwa njia ya
ubia Visiwani Zanzibar.

Bububu, Mahonda kupitia Kinyasini hadi Mkokotoni  ni Moja ya miongoni mwa
Mradi wa Ujenzi wa Bara bara Nne za Unguja uliotiwa saini mnamo tarehe 8
Novemba Mwaka 2017 hapo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” Mkokotoni na kushuhudiwa pia na Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Mradi huo unaojumuisha pia barabara za Pale - Kiongele,  Matemwe – Muyuni
pamoja na Fuoni – Kombeni zinazotarajiwa kuwa na Urefu wa Kilomita 52
unagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kupitia Mkopo nafuu wa
fedha wa shilingi Bilioni 58 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika 'ADB'.


Picha na Habari kwa hisani ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Wizara ya Mambo y Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ofisi ya Zanzibar

Post a Comment

0 Comments