NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri amewaagiza
viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) kuhakikisha vinatenga sehemu
ya mapato vitakayopata msimu huu wa mauzo ya tumbaku na pamba kwa ajili ya
kununulia matrekta.
Hatua hiyo inalenga
kuleta mapinduzi ya kilimo miongoni mwa wakulima ambao ni wanachama wao na wale
ambao sio wanachama.
Mwanri alitoa kauli
hiyo jana katika Wilaya ya Kaliua na Urambo alipokutana na wadau mbalimbali
wakiwemo watendaji wa vijiji, Kata , Maafisa Elimu Kata na walimu wakuu.
Alisema matumizi wa
mashine kama vile matrekta katika kilimo ndiyo yatakayowezesha wakulima mkoani
humo kupiga hatua na kupata ziada itakayotumika kuwaletea maendeleo na hivyo
kuwa na malighafi nyingini kwa ajili ya viwanda na matumizi mengine.
“Tunataka kila Chama
cha Ushirika cha Msingi kwa kutumia ile sehemu ya pesa kinachopata kwa kila
kilo inayouzwa kinunue trekta ili tuondokane na matumizi ya jembe la mkono
ambalo kwa kiasi kikubwa halitoi uwezo kwa mkulima kulima eneo kubwa katika
muda mfupi ambapo mavuno yake ndio yangempa ziada” alisema Mwanri.
Mkuu huyo wa Mkoa
alisema trekta hilo linaweza kutumika kama chanzo cha mapato kwa Chama cha
Msingi kuwakodishia wanachama wake na wasio wanachama wake wakati wa kulima na
wakati wa kusomba mazao mbalimbali kutoka mashambali.
Mwanri aliongeza kuwa
kilimo kitakapo kuwa cha kisasa na kilichochukua eneo kubwa wakulima wataanza
kufikia hata kutumia mashine kubwa katika uvunaji wa mazao yao mbalimbali.
Alisema sanjari na hilo ameagiza kuanzia sasa kila zao linalolimwa Mkoani
Tabora ni lazima lilimwe kwa kufuata mstari na pia mkulima atumie mbolea za
viwandani au samadi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri katika uzalishaji.


0 Comments