INSPEKTA Jenerali wa Polisi, Simon Sirro amewaonya watu waliopata msamaha
wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa Aprili 26, 2018 wajichunge tabia na matendo
yao.
Ametoa onyo hilo leo (Alhamisi, Mei 24, 2018) mbele ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo vya polisi vya kisasa vya Mburahati,
Kiluvya-Gogoni na Mbweni ambavyo vimezinduliwa leo.
Alisema nia ya Mheshimiwa Rais Magufuli kuwapa msamaha ilikuwa njema
lakini lakini kuna baadhi ya watu wameitumia vibaya fursa hiyo na hadi sasa watu
watano wamekwishauawa na wananchi.
“Mheshimiwa Rais aliwapa msamaha baadhi ya watu mnamo tarehe 26 Aprili
lakini wametumia vibaya msamaha na kurejea kwenye matendo yao maovu na hadi
sasa watu watano wamekwishauawa na wananchi,” alisema.
Alisema anatoa onyo kwa wote waliopata msamaha na wana nia ya kurejea
kwenye matendo yao maovu. “Ukitoka gerezani kwa msamaha, maana yake umerekebisha
mwenendo wako na wananchi wanatarajia uwe hivyo, lakaini kama ukifanya
vinginevyo, Serikali isilaumiwe,” alisema.
Akielezea kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda Sirro alisema tangu
ashike madaraka hayo, jeshi hilo limewapeleka askari 1,267 kwenye mafunzo ya
medani za kivita na kwamba jeshi hilo liko imara.
“Pia tumepeleaka askari wa upelelezi zaidi ya 1,000 kwenye mafunzo ya
ujuzi na ustadi (skills and knowledge) wa kupeleleza kesi mbalimbali. Baada ya
kuwapa mafunzo haya, tunataka kesi za kawaida upelelezi wake uwe umekamilika
ndani ya miezi sita na zile kesi kubwa kubwa upelelezi wake uwe umekamilika
ndani ya miezi 12. Tunataka kuhakikisha haki za Watanzania zinapatikana kwa
wakati,” alisisitiza.
Kamanda Sirro alitumia fursa hiyo kumshukuru pia Rais Magufuli kwa
kuwapatia sh. bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari; kutoa kibali
cha ajira kwa askari wapya 1,500 na kuwaruhusu wawapandishe vyeo askari wenye
kustahili kuanzia cheo cha Koplo hadi Naibu Kamishna wa Polisi (DCP).
0 Comments