Picha ya pamoja ya Wajumbe wa Bodi ya Parole pamoja na Mkuu wa Mkoa wa
Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa tano toka kushoto) nje ya jengo la ofisi
ya mkuu wa mkoa Rukwa.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameyaomba
mashirika binafsi kuona umuhimu wa kuwawezesha wafungwa wanaotoka magerezani
kupitia mpango wa ‘parole’ ili wafungwa waweze kupata kianzio cha maisha
wanaporudi uraiani kuendelea na maisha yao.
Amesema kuwa wafungwa wengi wanaotoka kwa mpango huo
wanakuwa wametumikia kifungo cha zaidi ya miaka minne gerezani na watokapo huwa
na ujuzi wa kuweza kujiajiri na kuweza kuendelea kulitumikia taifa katika
kukuza uchumi na kuacha kuwa tegemezi katika familia.
“Kumbuka kuwa wamekaa zaidi ya miaka minne hivyo wanapotoka
kule wanakuwa na changamoto kubwa sana ya kuanza maisha ingawa wanakuwa na
ujuzi wao, na wakati mwingine hata jamii inawanyanyapaa, kwahiyo Taasisi zisizo
za kiserikali ni vyema zikaunga mkono mpanpo huu ili kuwawezesha kuwapatia
kianzio cha maisha n ahata kukuza ujuzi walionao ili wajione ni sehemu ya
jamii,” Alifafanua.
Ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Parole Mkoa wa
Rukwa ambayo hudumu kwa miaka mitatu na Mwenyekiti wake aliteuliwa mwishoni mwa
mwaka 2017 na kumaliza muda wake mwishoni mwa mwaka 2020.
Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Magereza Mkoa wa
Rukwa ACP. Simon Ihunja amezitaja changamoto zinazowakumba wafungwa hao
wanapotoka gerezani huku kubwa likiwa ni kukosa kuwezeshwa wanapotoka magerezani
baada ya kutumikia vifungo vyao.
“Mpango huu huwavutia wafungwa na kuona umuhimu wa kukaa vizuri
gerezani ili waweze kutuliwa au kuchaguliwa kumalizia kifungo wakiwa nje,
changamoto inayowakumba ni ile ya kwamba wanapotoka wanakuwa hawana kianzio ya
kwamba anakwenda kuanza vipi wakati ameshatumikia miaka 10 hadi 15,” Alisema.
Bodi hiyo iliyozinduliwa ni bodi ya sita kutekeleza majukumu
yake tangu kuzinduliwa kwa bodi hiyo mara ya kwanza mwaka 2003 na hadi sasa
imewanufaisha wafungwa 176 ambapo mmoja wa wafungwa hao alivunja masharti ya
bodi hiyo na kukamatwa na kurudishwa tena gerezani.

0 Comments