Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, wakati alipotembelea
shamba la pamba la mzee Rashid Msilu huko Chalinze, Bagamoyo ambapo
alihimiza wakulima Mkoani humo kulima zao hilo .(Picha na Mwamvua
Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
WAKULIMA wa mazao ya kibiashara Mkoani Pwani, wamehamasishwa kulima kilimo cha pamba ili kujiinua kimaendeleo na uchumi .
Aidha
imekemea utoaji wa dawa za viuadudu vinavyoshambulia zao hilo ambazo ni
feki na kudai mtu atakaegawa dawa feki ,atachukuliwa hatua kali ,kwani
inasababisha kudididimiza juhudi za wakulima hao.
Mkuu
wa mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo alihimiza kilimo hicho,
wakati alipokwenda kutembelea shamba la pamba la mzee Rashid Msilu huko
Kweikonje ,Bagamoyo.
Alisema katika mkoa huo maeneo yanayostawi zaidi kilimo cha pamba ni wilaya ya Rufiji na Chalinze.
Ndikilo
alieleza, kipindi cha nyuma kilimo hicho kilitetereka lakini kwasasa
mazingira na ardhi inaruhusu kuinua kilimo cha zao hilo.
Kwa
mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, kupitia wizara ya kilimo imeshasambaza
mbegu bora ya pamba,mabomba ya kupulizia dawa kwa mkopo na dawa za
viuadudu zimetolewa bure.
Ndikilo
alifafanua, Chalinze imeshapatiwa lita 226 za dawa za kupulizia kuzuia
wadudu waharibifu ,Rufiji imepewa lita 120 ambapo mabomba ya kupulizia
dawa yametolewa 40 kwa ajili ya Chalinze na Rufiji mabomba kumi.
Aliomba dawa hizo ziwafikie wakulima wa pamba ili kuleta tija.
"Kuhusu
dawa feki ,nimesikia kwa baadhi ya wakulima kuwa mwaka jana zililetwa
dawa feki ,hazikuuwa wadudu,kwakweli kipindi hiki sitokubali kusikia
tatizo hilo tena" alisisitiza Ndikilo.
Pamoja na hayo , alikemea pasiwepo na hujuma yeyote wakati wa hatua ya uvunaji .
"Kuna
baadhi ya wakulima wanaweka maji ,mawe ,mchanga kwa lengo la kuongeza
uzito ,;msifanye hivyo mnashusha sifa ya mkoa na Taifa ".
Ndikilo
alisema pia, vyama vya msingi viwe na maghala ,mizani halali na
vifungashio bora ili kupeleka vyama vya ushirika kupata masoko ya
uhakika.
Alielezea mwaka
jana alisikia chama cha ushirika -Corecu hakikuchukua pamba za wakulima
kutokana na kukosa fedha ,hivyo aliwahakikishia wakulima ataongea na
mwenyekiti wa Corecu kuangalia namna ya kununua pamba hizo .
Nae
ofisa Kilimo,Umwagiliaji na Ushirika Chalinze Jovin Bararata ,alisema
halmshauri ya Chalinze ni moja ya halmshauri zinazolima pamba Mkoani
hapo .
Alibainisha, mwaka jana walivuna tani 63 na mavuno yajayo wanatarajia kuvuna tani 250.
Bararata
alielezea ,wamejiwekea mikakati ya kuhamasisha kilimo hicho ambapo
wamenunua pikipiki 15 ambazo watagawiwa maafisa ugani ili waweze
kuwatembelea wakulima mbalimbali kirahisi .
Mkakati
mwingine ni kukabiliana na tatizo la soko kwa kuimarisha vyama vya
msingi ili kuhakikisha vinaratibu vizuri na kukusanya pamba":, wakulima
waweze kunufaika na mfumo wa stakabadhi ghalani.
Bararata
alisema ,ipo changamoto ya wadudu waharibifu na panya ambapo
wanadhibiti hali hiyo kwa kushirikiana na bodi ya pamba kwa kuhakikisha
dawa zinagawiwa kwa wakati.
Mkulima wa pamba , mzee Rashid Msilu aliishukuru serikali kwa kuwapatia dawa,mbegu bora ili kulima kisasa.
Nchi
ya Tanzania inaingiza fedha nyingi za kigeni kwa mazao ya biashara
makubwa matano ikiwemo kahawa, chai, korosho,pamba na Tumbaku lakini zao
linaloongoza kuingiza fedha hizo ni korosho.
Kwa
mkoa wa Pwani ,zao la biashara linaloingiza fedha za kigeni ni korosho
ambapo kwasasa serikali Mkoani humo inahimiza pamba ili kuwa na mazao
mawili ya kibiashara.


0 Comments