Random Posts

Visiga Yakabiliwa na Mlundikano wa Wanafunzi na Uhaba wa Madawati

 Diwani kata ya Visiga ,Kambi Legeza akizungumza jambo kuhusiana na sekta ya elimu kwa wakazi wa Visiga.
Wakazi wa kata ya Visiga wakimsikiliza Diwani wa kata ya Visiga ,Kambi Legeza hayupo pichani.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WANAFUNZI wa shule ya Msingi Visiga,Kibaha mkoani Pwani wanakabiliwa na changamoto ya mlundikano madarasani kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa 30 na madawati hali inayosababisha baadhi yao kukaa chini.
Aidha kila darasa kuna idadi ya wanafunzi 170 suala ambalo ndilo linalosababisha uhaba wa madawati na mlundikano huo.
Akielezea tatizo hilo katika mkutano wa wazazi na wananchi, diwani wa kata ya Visiga, Kambi Legeza alisema changamoto zimekuwa kubwa kutokana na mwitikio mkubwa wa wazazi kupeleka watoto wao shule, kwa kuunga mkono agizo la serikali la elimu bila malipo .
Alieleza moja ya shule kwenye kata hiyo inayokabiliwa na changamoto hiyo ni shule ya Msingi Visiga ambayo ndiyo shule kubwa na yenye wanafunzi wengi kwenye kata hiyo.
Legeza alisema ,changamoto hiyo imeisukuma na kuulazimu uongozi wa kata hiyo ,kuitisha mkutano huo wa wananchi ambao umeridhia kila kaya kuchangia kiasi cha sh.4,000 ili kupunguza changamoto zilizopo kwenye shule za kata ya Visiga ikiwemo shule hiyo.
“Tumekubaliana  kila kaya ichangie kiasi hicho kwa ajili ya kuondoa changamoto za vyumba vya madarasa , upungufu wa madawati na matundu ya vyoo ” 
“Suala la kuchangia maendeleo ya elimu siyo kosa tatizo watu wanashindwa kuelewa michango mashuleni ndiyo imekatazwa lakini wananchi hawajakatazwa kuchangia kwa hiari yao kuondoa changamoto zilizopo ” alisema diwani huyo .
Hata hivyo ,Legeza alielezea jukumu la kutatua changamoto za kielimu ama maendeleo ya kijamii ni la jamii yenyewe badala ya kuitegemea serikali pekee.
Alisema kwasasa ,watafuata taratibu za kuomba kibali halmashauri na wilaya na fedha za mchango huo zote zitaingizwa kwenye mfuko wa elimu wa Halmashauri.
Nae mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Visiga  Moshi Mnaki alisema, changamoto za uhaba wa madarasa inasababisha wanafunzi kusoma kwenye mazingira magumu.
Alisema yapo madarasa mawili kongwe yaliyojengwa mwaka 1983 ambayo wanahitaji kuyakarabati na inatakiwa mil. Tisa ili kukamilisha ukarabati huo.
Mnaki alisema, darasa moja linafikia wanafunzi 170  ikiwa na idadi ya wanafunzi 1,350.
Mnaki alisema vyumba vya madarasa vilivyopo 11 mahitaji yakiwa ni 30 .
Changamoto nyingine ni upungufu wa matundu ya vyoo, ambapo  mahitaji yake ni 53 na vilivyopo 28 ,mapungufu 25.
Mnaki alielezea, madawati mahitaji 395 yaliyopo 317 ,upungufu 78 ,meza za walimu mahitaji 34 ,zilizopo 9 ,pungufu 29 ,viti mahitaji ni 34, na vilivyopo 19.
Mkazi wa Visiga ,Saidi Mtende alisema wamekubaliana kuchangia 4,000 kuondoa changamoto za kielimu .
Alisema ,wazazi wasikumbatie watoto wao na kuwageuza mabwana wakubwa kwa kuwaacha majumbani pasipo kuwapeleka mashuleni kupata elimu .

Post a Comment

0 Comments