Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Isaack Kamwelwe akisisitiza jambo kwa wataalamu
alipotembelea mradi wa maji Iyula halmashauri ya Mbozi, kushoto kwake ni Kaimu
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya maji Mkoa wa Songwe Mhandisi Tanu Deule.
Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Isaack Kamwelwe akikagua chanzo cha maji Itaka katika
halmashauri ya Mbozi pamoja na wataalamu wengine kutoka ngazi ya mkoa na
wilaya.
Na Grace Gwamagobe-Songwe
Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Isaack Kamwelwe ametahadharisha kuwafukuza kazi na kuwashitaki
wahandisi wa serikali wanaokosa uzalendo na kuhujumu miradi ya maji katika
hatua ya usanifu na usimamizi kwa kupitisha vifaa vilivyo chini ya viwango.
Mhandisi Kamwelwe
ametoa tahadhari hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Songwe ya kukagua utekelezaji
wa miradi mitatu ya maji ya Iyula na Itaka katika halmashauri ya Mbozi, mradi
wa Umwagiliaji Naming’ongo katika halmashauri ya Momba na mradi wa Maji Tunduma
katika halmasahuri ya Tunduma.
“Miradi mingi inakamilika
na kuzinduliwa na viongozi wakubwa wa kitaifa lakini mabomba yanaanza kupasuka muda
mfupi tu baada ya wananchi kuanza kupata maji kwakuwa hayana viwango, wahandisi
badilikeni na hili likitokea hauna ajira na kushitakiwa juu”, amesisitiza
Kamwelwe.
Ameongeza kuwa kukamilika
kwa miradi ya maji hakutakuwa na tija endapo shughuli za utafiti wa vyanzo
vingine imara vya maji hazitafanyika pamoja na kutunza vyanzo vya maji
vilivyopo kwa ajili ya uendelevu wa miradi hiyo kwa muda mrefu.
“Hatutaki kusikia
mradi unatoa maji kwa muda mfupi kisha maji yanaisha kwenye vyanzo, hivyo naagiza
taasisi ya bonde la ziwa Rukwa washirikiane na taasisi nyingine pamoja na ofisi
za wakuu wa wilaya kutafuta vyanzo vingine vya maji pamoja na ulinzi wa vyanzo
vilivyopo”, amebainisha Mhandisi Kamwelwe.
Kwa Upande wao
wananchi wameiomba serikali kuwepo kwa uwazi na ushirikishwaji katika hatua
zote za ujenzi wa miradi tangu hatua ya usanifu ili kujenga uelewa juu ya miradi
hiyo na kuondoa migogoro.
Ujenzi wa miradi ya
maji ya Iyula, Itaka na Tunduma inatarajiwa kutoa huduma ya maji kwa wananchi
takribani laki moja ambao watakuwa wanapata maji kwa umbali usiozidi mita 400
sawa na mwongozo wa sera ya maji ya mwaka 2002.


0 Comments