Subscribe Us

header ads

AQRB Imesema Migogoro Katika Sekta ya Ujenzi Inasababisha Miradi Mingi Kutokamilika kwa Wakati.

 Kaimu msajili wa bodi ya AQRB, Albert Munuo akizungumza na  wabunifu,  wakadiriaji majenzi na  wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi wakati wa mafunzo endelevu ya kuwajengea uwezo katika sekta hiyo. 
 Wadau wa sekta ya ujenzi wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Picha ya pamoja.

Habari Picha/ na Philemon Solomon
.........................................
BODI ya Usajili wa Wabunifu na Wakadiriaji Majenzi  AQRB imesema migogoro  katika sekta ya ujenzi inasababisha  miradi mingi kutokamilika kwa wakati  sambamba na kuwezesha kushindwa kujua thamani halisi ya ujenzi. 

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada kumalizika kwa  mafunzo yaliyoandaliwa na AQRB na  kuwakutanisha wabunifu,  wakadiriaji majenzi na  wadau mbalimbali wa sekta ya ujenzi mwishoni mwa wiki Kaimu msajili wa bodi hiyo Albert Munuo alisema mafunzo haya ni muendelezo wa taratibu zao ambapo wataalamu wamekuwa wakikutana mara mbili kwa mwaka na kujadili mada mbalimbali.

" Leo tumejadili migogoro mbali mbali ambayo hujitokeza katika sekta ya ujenzi na athari zake ambapo tumebaini kwamba migogoro hiyo  mbali na kusababisha gharama za ujenzi kuwa juu pia imekuwa ikisababisha miradi mingi kushindwa kukamilika kwa wakati,'"alisema Munuo. 

Alizitaja sababu zinazosababisha migogoro katika sekta ya ujenzi kuwa ni pamoja na kutokamilika kwa nyaraka za ujenzi kikamilifu ikiwepo michoro sambamba na mwenye mradi kutomlipa mkandarasi na mtaalamu mshauri kwa wakati.

Alisema yapo matatizo mengine ambayo husababishwa na washauri wasimamizi kwa kushindwa kutoa maelekezo ya kitaalamu kwa wakati kwa mkandarasi. 

' Kwa kuzingatia mjadala wote wataalamu tuliokutana tumeona ipo haja kila mtu kutimiza majukumu yake ili kuondoa migongano na kwa hili ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe kwa wataalamu watakaoenda kinyume cha taratibu,"alisisitiza Mumuo

Akizungumzia uhaba wa wataalamu wa fani ya ubunifu na ukadiriaji majenzi alisema hauendani na uhitaji na kwamba kwa sasa wanaotambulika ni 1,500 tu.

Alisema kutokana na hali hiyo AQRB imekuwa ikihamasisha vijana kupitia programu maalumu ambapo wataalamu wamekuwa wakipita mashuleni kuanzia shule za sekondari kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi ili baadae waweze kusoma fani hii na kulipunguzia taifa uhaba wa wataalamu hao.

Pia alisema ili kuondoa mkanganyiko uliopo baina ya wataalamu wa ubunifu,wakadiriaji majenzi na wahandisi  wameandaa mpango mkakati maalumu wa kuielima jamii utofauti wa majukumu ya wataalamu hao huku akihimiza kuwataka watanzania kubadilika na kuwatumia wataalamu katika ujenzi mbalimbali ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kukosa ushauri kutoka kwa wataalamu hao.

Hata hivyo Munuo aliwaomba wataalamu wenye makampuni kuwachukua vijana wanaotoka vyuoni na kuwapa kazi ili waweze kupata uzoefu wa fani walizosomea.

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye aliwasilisha mada inayohusu jinsi ya kuzuia migogoro ya sekta ya ujenzi Wakili Madeline Kimei aliunga mkomo suala la vijana wanaotoka vyuoni kupewa kazi na wenye makampuni kwa kusema kuwa kupatiwa kazi kwa vijana hao kutawahamasisha na kuwapa uzoefu wa kazi.