(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa)
Jeshi la Magereza nchini limepongezwa kwa kubuni utaratibu mzuri wa kujiendesha kimapato kupitia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba bora kwa gharama nafuu.
Pongezi hizo zimetolewa mwishoni
mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti, wakati akizindua mradi wa
nyumba za kuishi askari na mradi wa maji kwenye Gereza la Kilimo Mollo Wilaya
ya Sumbawanga.
Mkirikiti alifurahishwa
kuona mradi wa nyumba ya kuishi familia mbili iliyojengwa kwa sh. mil 55 na
aliwapongeza kwa kutekeleza dhana ya Magereza ya kujigemea kwakuwa inaongeza
tija kwa Mkoa kupitia miradi inayotekelezwa.
“Kama Magereza imeweza kujenga
nyumba moja ya famili kwa gharama ya sh mil 57, huu ni mfano mzuri wa ubunifu. Wito
wangu kwa Halmashauri za Rukwa ziige mfano huu kwenye utekelezaji miradi ya
ujenzi ili kupunguza gharama za fedha za Serikali “alisisitiza.
Awali akitoa taarifa ya miradi,
Mkuu wa Gereza la Kilimo Mollo,Mrakibu wa Magereza (SP) Nicostratus Magori, alisema
mradi wa nyumba za kuishi askari umetekelezwa kwa lengo la kupunguza uhaba wa
makazi bora ya askari .
Aliongeza kusema gharama halisi
za mradi wa nyumba hiyo ni sh. mil 55 ambapo gereza kupitia miradi yake limechangia
sh. mil 17.3 na Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) alichangia sh. mil 38.
Kuhusu mradi wa maji safi
na salama SP Magori alisema shil mil 7.6
imetumika kufufua mradi huo ambapo fedha zote zimetokana na miradi ya Gereza la
Mollo.
SP Magori alitoa ombi kwa
Mkuu wa Mkoa kuwa Gereza lisaidie kupata miradi mbalimbali kwa kuwa lina nguvu
kazi na utaalam, hatua itakayosaidia kutekeleza miradi kwa ubora huku gereza likiongeza
uwezo wake wa kujitegemea kimapato.
“Miradi hii licha ya
kutuimarisha kiuchumi, inasaidia pia kutoa mafunzo ya ujuzi kwa wafungwa ili
watakapomaliza vifungo vyao itawasaidia kuwa raia wema kwa kufanya kazi halali
za kujitegemea” alisema SP Magori.
Gereza la Kilimo Mollo
lilianzishwa mwaka 1967 na lina eneo la ekari 8,989 na kwa sasa lina miradi ya ujenzi wa
nyumba ya kulala wageni, ujenzi wa bwalo, ujenzi wa fremu 11 za maduka na
ujenzi wa viwanda vidogo vya kuchakata mazao ya ngano, alizeti na mahindi.

0 Comments