Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza leo na wananchi wa vijiji vya Mpambaa Wilaya ya Singida na Kinampundu Wilaya ya Mkalama kusuluhisha mgogoro wa ardhi wa Shamba la Mbegu la Mpambaa .
.........................................
Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amemaliza mgogoro wa shamba la mbegu lenye ukubwa wa ekari 456.82 lililopo kati ya kijiji cha Mpambaa Wilaya ya Singida DC na kijiji cha Kinampundu Wilaya ya Mkalama kwa kuagiza wananchi wagawiwe shamba hilo mara moja.
Alitoa agizo hilo leo akiwa na viongozi wa wilaya za Mkalama na Singida wakati akizungumza na wananchi wa vijiji hivyo ambao tangu mwaka 2020 kumekuwa na mgogoro hyo huku kila upande ukidai una haki ya kumiliki shamba hilo ambalo lilikuwa chini ya serikali ya Mkoa wa Singida.
"Naagiza shamba lote ekari 456.82 lenye mgogoro ligawanywe kwa wananchi wa Halmashauri za Wilaya ya Singida Vijijini na Halmashauri ya Wilaya Mkalama kwa kuzingatia mipaka iliyoainishwa kwenye GN," alisema.
Serukamba alitoa mchanganuo kuwa ekari 222.5 ambazo zipo upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama zigawiwe kwa wananchi na ekari 234.32 zigawiwe kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya Singida.
Kufuatia maamuzi hayo, Mkuu huyo wa Mkoa alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Singida,Paskas Mlagiri na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigho,wasimamie ugawaji wa mashamba hayo ili wananchi wanufaike kwa kuendeleza kilimo,ufugaji na shughuli ngingibe za uzalishaji mali.
Alisema vijiji vilivyopo eneo la mashamba haya vipewe kipaumbele cha kuandaliwa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kuepuka mgogoro mingine ndani ya utawala wa vijiji.
Aidha, aliagiza kuwekwa alama za mipaka (beacon) maeneo ya karibu mita 100 hadi 200 kwenye maeneo ya mpaka na wananchi wapewe elimu walipo na pia halmashauri na serikali za vijiji zihakikishe watakaopewa mashamba wanayalima na sio kuyaacha kuwa mashamba pori.
"Tusisubiri mgogoro kama hii inaibuka na kufika mpaka ngazi ya mkoa, wizara na ofisi za viongozi wa kitaifa ilhali sisi hatuna taarifa,tuishughulikie kwa kadri ya uwezo wetu ili tuitatue na wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku za kujenga nchi," alisema.
Akielezea historia ya mashamba hayo, alisema huko nyuma Mkoa wa Singida ulianzisha mashamba makubwa mawili, shamba A na Shamba B ambayo yalikuwa maalum kwa ajili ya kuzalisha mbegu.
Alisema shamba moja lilikuwa upande wa Singida na jingine lilikuwa upande wa Wilaya ya Iramba ambapo Wilaya ya Singida iliamua shamba A walipime na kulitolea hati hivyo likabaki ni mali ya Singida lakini shamba B halikupimwa wala kupewa hati na wananchi waliendelea kulima bila utaratibu wowote..
Serukamba alisema mgogoro ulianza mwaka 2012 baada ya serikali ilipoanzisha Wilaya mpya ya Mkalama ambapo shamba B wananchi wa Wilaya ya Singida na wa Mkalama walianza kugombaniana kila upande ukisema ni yake.
"Kwa kawaida ndugu wananchi tukiunda wilaya lazima wilaya iwe na mpaka wake,lazima tutowe GN ili kila wilaya ijue mipaka yake kwa hiyo Iramba ikasogezwa mbali na ilipochorwa ramani kutengeneza mpaka shamba B likawa katikati ya wilaya ya Singida na Mkalama.
Alisema kufuatia mgogoro wa wananchi wa pande zote mbili, serikali iliunda tume kuchunguza suala hilo na kuja na majibu kuwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida wagawiwe ekari 234.32 na wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wapewe ekari 222.5 ili kumaliza mgogoro huo.
" Utatuzi wa migogoro ni suala ambalo lazima tuangalie sheria,kanuni na miongozo inasemaje na sio suala la kukurupuka," alisema Serukamba.
Aliomgeza kuwa kwa kuwatumia wataalam waliopitia mipaka ya kisheria kwamujibu wa GN Na.160 ya 15/11/1935 ,GN namba 287 ya 9/9/2011 zinazohusu Halmashauri ya Wilaya ya Singida na tangazo la uanzishwaji Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama la 26/6/2013 na kuwashirikisha wananchi na kukubaliana uwandani kuhusu mipaka halisi ya eneo la shamba na mipaka ya maeneo ya utawala (wilaya).
Wananchi kwa upande wao walipongeza maamuzi yaliyofikiwa na Mkuu wa Mkoa na kwamba mgogoro sasa umefikia tamati wanachokisubiri ni watalaam kwenda kuwapimia ili waendelee na shughuli za kilimo.



No comments:
Post a Comment