Na Dotto Mwaibale, Singida
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeanza kutoa elimu ya Nishati
ya Umeme Jua katika vyuo vyake vyote nchini ikiwa ni moja ya njia ya kuunga
mkono jitihada za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassanza kuhakikisha
nchi inapata umeme wa uhakika.
Akizungumza Oktoba 27, 2023 , wakati akifunga mafunzo ya nishati ya umeme
jua ya wiki mbili kwa walimu wa vyuo 12 vya VETA ambayo yameandaliwa na VETA
Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Mkurugenzi wa
VETA Kanda ya Kati, John Mwanja alisema mafunzo hayo ni ya muhimu hasa katika
kipindi hiki ambacho nchi inamgawo wa umeme na inafikiria kuiwasha kwa kutumia
umeme huo kupitia wataalamu waliozalishwa na VETA.
“VETA ndio tumepewa majukumu ya kutoa elimu hii kwenye vituo vyetu na
kuhakikisha watanzania wote waliopo mijini na vijijini wanaipata,” alisema
Mwanja.
Mwanja alisema kupitia wahitimu hao sasa VETA inakwenda kupata walimu wa
kufundisha kozi hiyo na kuwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA aliwaomba wakuu wa vyuo
katika kanda zao kuwaruhusu walimu kuhudhuria mafunzo hayo.
Alisema mafunzo hayo yalianzishwa VETA Mkoa wa Singida ambapo awamu ya
kwanza na ya pili yamefanyika hapo na kwa awamu hii waliona yasihusishe watu wa
kutoka Singida pekee bali uongezwe wigo wa kuwapata wengi lengo likiwa yasambae
kila sehemu ambapo VETA ipo.
Alisema ilipendekezwa hivyo si kwa ajili ya kupata watu wengi bali viwepo
vituo vingine kama cha Singida kwenye vyuo vingine kwa ajili ya kupata elimu na
wataalam kwenye maeneo hayo.
Alisema kama inavyofahamika majukumu ya VETA ni kufundisha ujuzi na kuwa
elimu hiyo ya nishati ya umeme jua ni muelekeo na mpango wa Serikali kutokana
na kuwepo kwa changamoto kubwa ya umeme na kuwa moja ya maono ya Serikali ni
kuona nchi inapata umeme kutokana na mfumo wa jua.
Alisema wanapotegemea kupata umeme kupitia mfumo huo ni lazima wawepo
wataalam wa kutosha wa kufanya kazi hiyo na kuwa kuna wadau wengi kama Chuo cha
Ufundi Arusha (ATC) ambao wanafundisha kozi hiyo lakini na VETA wanaowajibu wa
kuiunga mkono Serikali wanapotaka kuongeza nishati hiyo kwa kuhakikisha wataalam
wanapatikana.
“Haiwezekani wataalam hao wapatikane kwa kutumia kituo cha Singida peke
yake hivyo VETA kama wajibu wetu ni lazima wataalam hao wasambae nchi nzima,”
alisema Mwanja.
Alisema mahitaji ya VETA ni kutaka kijana aliyopo kule Busokelo mkoani Mbeya
au Mwanza na maeneo mengine ya nchi wapate elimu hiyo katika vyuo vilivyopo
katika maeneo yao badala ya kwenda Singida jambo litakalowapunguzia gharama na
ndio maana Serikali inajenga vyuo vya VETA kila wilaya kwa lengo hilo na kuwa
jukumu lao ni kupeleka huduma kwa watumiaji na wadau wao ambao ni hao wanafunzi.
Mwanja alisema kutokana na hali hiyo VETA iliona licha ya kozi hiyo kuanza
kutolewa Mkoa wa Singida sasa itolewe katika Mikoa yote kupitia vyuo vya VETA
ikiwa ni kuwasogezea huduma watanzania.
Aidha, Mwanja aliwataka wahitimu hao mara watakaporudi kwenye vituo vyao
wakawe na mwendelezo wa kwenda kutoa elimu hiyo ambayo pia wanafunzi
wanaojifunza fani ya umeme wa kawaida katika chuo hicho wameyapata.
Katika hatua nyingine Mwanja alivitaka vyuo hivyo kujitangaza ili shughuli
wanazozifanya zifahamike ikiwa ni pamoja na mafunzo ya nishati ya umeme jua jambo
litakalosaidia kufahamaika na akahimiza pia kuanzisha kozi fupi za mafunzo
hayo.
“Suala la kujitangaza ni la muhimu tumieni mitandao ya kijamii kuna chuo
kimoja kule Ruvuma nilikuta kuna raia wa kigeni kutoka nchi jirani ikiwemo
Msumbiji wapo kupata mafunzo
nilipouliza walijueje kama kuna hicho chuo walisema kupitia matangazo
hivyo ndugu zangu tangazeni vyuo vyetu kwani biashara ni matangazo,” alisema
Mwanja.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Singida, Alphonsina
James aliwashukuru washiriki wa mafunzo hayo kwa ushirikiano mkubwa
waliouonesha wakati wa mafunzo na kueleza kuwa kwao ni bahati kubwa kwani
katika vyuo 48 ni vyuo 15 pekee ndio vilivyotoa washiriki hao.
Katika risala ya wahitimu hao kwa mgeni rasmi waliomba muda wa mafunzo uongezwe pamoja na uratibu wa mafunzo hayo ufanywe na VETA makao makuu kwa ajili ya uwezeshwaji ambapo pia waliomba kuwezeshwa vifaa vya kufundishia.
0 Comments