Na Dotto Mwaibale, Singida
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Dk.
Binilith Mahenge ameendelea kuwahimiza wawekezaji kusajili kazi zao za biashara
wanazozifanya ili waweze kutambulika na kupata fursa mbalimbali.
Dk.Mahenge ametoa ombi hilo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na
viongozi wa mgodi wa uchimbaji madini wa Shanta uliopo Wilaya ya Ikungi na
baadhi ya wawekezaji wa Mkoa wa Singida alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi
ya kampeni ya kuhamasisha uwekezaji, kukutana na wawekezaji na kujua changamoto
walizonazo ili kuzitafutia ufumbuzi.
Alisema hivi sasa suala la uwekezaji ni la muhimu si kwa Tanzania peke yake
bali kwa dunia nzima ambapo katika kila nchi kumekuwa na makongamano
yakifanyika ya kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji.
"Uwekezaji hivi sasa kila mahali pote duniani ni ushindani ukienda
uchina, Marekani, Urusi, India wanataka wawekezaji na kila wiki makongamano
yanafanyika kwa ajili ya kutangaza vivutio walivyo navyo ili kutafuta
wawekezaji ni jambo ambalo tunanyang'anyana," alisema Dk.Mahenge.
Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu tulimsikia aliposema Serikali peke yake
haiwezi kuleta maendeleo katika nchi ni lazima ishirikiane na sekta binafsi
ambapo wanapatikana wawekezaji.
Alisema TIC wamepewa dhamana na Serikali ya kuhamasisha uwekezaji pamoja na
kuusajili kutokana na umuhimu huo ndio maana wanafanya ziara ya kuwatembelea
kuona kazi wanazozifanya, kujua changamoto zao na kuwahamasisha wazisajili.
Alisema TIC imeanzisha kampeni ya kuhamasisha wawekezaji wa ndani
kujisajili na kujulikana ili nao wapate faida kama wanayoipata wawekezaji
wengine kutoka nje ya nchi kwani wengi wao hawajasajiliwa na wengine
hawajulikani kabisa.
Kaimu Meneja wa mgodi wa uchimbaji wa madini wa Shanta Reuben Ngusaru
akizungumza katika kikao na Mwenyekiti huyo na ujumbe wake alisema moja ya
changamoto kubwa walionayo ni ukatikaji wa umeme mara kwa mara hivyo kufifisha
utendaji wa kazi kwa ufanisi na uzalishaji.
“Tuna jenereta letu lakini tukiliwasha kwa masaa 12 ni sawa sawa na kutumia
umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa siku sita hiyo ni gharama ya
mafuta na hivi sasa tupo kwenye mgao wakati mwingine tunakuwa kwenye mgawo huo
kwa saa 12 na hii robo ya mwaka ya nne hata maduhuli yatapungua na hii ni
changamoto kubwa sana kwetu,” alisema Ngusaru.
Ngusaru alitaja changamoto nyingine ya kisheria ni suala la sera mpya ya
Serikali ya kubakisha asilimia 40 ya fedha katika Kata ya Mang’onyi ulipo mgodi
na asilimia 60 kupelekwa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.
Alisema kiwango hicho ni kikubwa mno kwao kutokana na kuanza kazi hiyo ya
uchimbaji muda mfupi uliopita na kuwa kiwango hicho kilipaswa kutolewa kwa
wachimbaji wa muda mrefu.
Ngusaru alisema kwa wananchi wa vijiji vilivyopo jirani na mgodi huo sio rahisi
kuelewa labda tu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo aende kutoa elimu kwa wananchi
hao ambapo aliomba jambo hilo lianghaliwe kwa jicho la karibu.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TIC, Mhandisi Peter Chisawillo,
aliupongeza uwekezaji wa mgodi huo ambao kazi nyingi zinafanywa na watanzania
za kuendesha mitambo na teknolojia zingine hadi kupatikana kwa dhahabu na
kueleza kuwa inaonesha thamani ya elimu walioipata na kuwa ni faida kwa nchi.
Dk.Mahenge akihitimisha ziara yake kwa kufanya kikao na wawekezaji wa Mkoa
wa Singida alisema una fursa nyingi za uwekezaji na akaipongeza Halmashauri ya
Wilaya ya Ikungi kwa kuandaa mipango mizuri ya uwekezaji kwa kutenga maeneo na
kupima ardhi ambapo aliziomba halmashauri zingine kuiga mfano huo.
Baadhi ya wawekezaji walioudhuria kikao hicho walieleza changamoto kadhaa
walizonazo ni kuto thaminiwa na taasisi zingine kwa kurundikiwa kodi nyingi na
kuorodheshewa makosa ya kulipa faini ambapo
waliomba wajengewe mazingira rafiki ili nao waweze kukua na kuwa wawekezaji
wakubwa.
No comments:
Post a Comment