Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam imeandaa kikao kazi na wadau wake wa mkoa wa Pwani kilichofanyika mkoani Pwani – Wilayani Kabaha katika Chuo cha Mwalimu Nyerere kuzungumza kwa pamoja namna ya koboresha upatikanaji wa bidhaa za afya.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt. Urio Kusirye amesema vikao kazi hivi ni muhimu kwani vinachangia kuhakikisha huduma za afya ndani ya Mkoa wa Pwani zinakuwa endelevu na bora.
“Tunapaswa kuwa na vikao kama hivi ili kuhakikisha changamoto zote ambazo zinajitokeza katika utendaji wetu wa kila siku zinazungumzwa kwa pamoja na kutatuliwa kwa pamoja”.
Hata hivyo, Dkt. Kusirye ameongeza kuwa ukilinganisha tulikotoa na tulipo sasa MSD kwa kiasi kikubwa imeboresha huduma zake akieleza kuwa bidhaa za afya ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana kwa kiasi kidogo sasa zinapatikana vizuri kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
“Tunakubali kuwa tunachangamoto kadhaa za kiutendaji ambazo zinaweza kutatuliwa kwa kukutana sisi kwa pamoja na kuwekeana mikakati ya namna ya kutatua changamoto hizo.” Aliongeza Dkt. Kusirye.
Naye Meneja Kanda ya Dar es Salaam Bi. Betia Kaema amesema kwenye kikao hicho wamewekeana maazimio na wadau wao ambao wanawahudumia wa Mkoa wa Pwani, ambapo maazimio hayo yatakuja kupimwa mwaka wa fedha ujao ili kujua yale yaliyofanyiwa kazi.
Wadau wakichangia michango yao ya namna ya kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya katika mkutano huo.Mkutano ukiendelea
0 Comments