Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa (katikati) akiongoza kukata keki maalumu ya Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja duniani 2024 Mkoa wa Singida yalioanza leo. Kulia ni Mwanachama wa mfuko huo, Yohana Julius na kushoto ni Afisa Huduma kwa Wateja NSSF Mkoa wa Singida, Latifa Singano.
............................
Imeandaliwa na Mtandao wa Singidaniblog
WANACHAMA wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wametakiwa kujenga utamaduni wa kufuatilia na kuhakiki taarifa za michango yao mara kwa mara wakiwa kazini badala ya kusubiri wakiwa wamestaafu.
Ombi hilo
limetolewa Oktoba 7, 2024 na Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa ambaye
alikuwa mgeni rasmi wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja
duniani 2024 Mkoa wa Singida.
“Niwakumbushe wanachama wetu kuhakiki taarifa za michango wanapokuwa kazini
ili kuepuka usumbufu wa kufuatilia michango yao wanapokua tayari wamestaafu au
kuwa nje ya ajira kwani jambo hili huwaletea usumbufu, kukosa ushirikiano
kutoka kwa baadhi ya waajiri wao na hivyo kuleta chuki baina ya wanachama na
Mfuko pale wanaposhindwa kulipwa mafao kwa wakati,” alisema Kalimilwa.
Kalimilwa alisema wiki ya huduma kwa wateja ilianzishwa rasmi
kimataifa mwaka 1987 kwa lengo la kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja na
juhudi za wafanyakazi wanaotoa huduma bora kwa wateja.
Alisema
kwa mwaka huu 2024 maadhimisho hayo yanaanza leo Oktoba 07, 2024 na yatafikia
tamati Oktoba 11, 2024.
“Tunatambua mchango mkubwa wa wateja wetu katika kuwezesha mfuko wetu kuendelea kufanya shughuli zake kuu nne ambazo ni Uandikishaji wa wanachama, Ukusanyaji wa michango, Ulipaji wa mafao pamoja na Uwekezaji,”. alisema Kalimilwa.
Alisema
pamoja na mambo mengine, mfuko hutumia maadhimisho hayo ya wiki ya huduma kwa
wateja kutoa shukrani kwa wateja kwa kutambua mchango wao katika kukuza mfuko
huo na kuwa ni wazi kuwa uendelevu na ustahamilivu wake unategemea wateja.
“ Naomba
kuwaahidi kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini kwamba Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya
Jamii (NSSF) utaendelea kutoa huduma bora zaidi popote wateja wetu walipo na tutawafikia kidigitali zaidi,”
alisema Kalimilwa.
Akizungumzia
hali ya mfuko kwa sasa alisema hadi
kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/2024 mfuko ulikuwa na wanachama
1,354,985 na waajiri 43,430 na kuwa kwa
mwaka wa fedha 2023/2024 mfuko uliandikisha wanachama wapya 291,266 huku
wakijiwekea malengo ya kuandikisha
wanachama wapya 324,321 kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Alisema kutokana na hali hiyo ni dhahiri kuwa mfuko unakua kwa kasi hivyo ni
lazima kasi ya ukuaji wa mfuko iende sambamba na ubora wa huduma zinazotolewa
na mfuko kwa wanachama wao.
Akizungumzia
wajibu wa watumishi wa mfuko huo alisema wana
kazi kubwa ya kuhakikisha wanafikia matarajio ya wateja na wadau wao
ikiwa ni pamoja na wastaafu wanaopokea pensheni, wanachama waliopo sasa na wa
baadaye lakini pia Serikali kwa kutoa huduma bora na rafiki na kwa kuzingatia
hilo, mfuko umewekeza katika kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kuwafikia wanachama
wake kwa urahisi na kwa haraka popote walipo.
Aidha, Kalimilwa
alisema sasa mfuko umeshakamilisha taratibu zote za uanzishwaji wa mfumo wa
ufunguzi na malipo ya mafao kupitia mtandao na huduma hiyo imeshaanza kwa
baadhi ya mikoa.
“Huduma
hii inatoa fursa kwa wanachama walioko mbali na matawi yetu kuweza kufungua
madai mahali popote walipo, kufuatilia maendeleo ya ulipaji na hatimaye kulipwa
kwa mujibu wa kanuni za ulipaji wa mafao,” alisema Kalimilwa.
Aidha,
kwa sasa Mfuko umeshakamilisha taratibu zote za uanzishwaji wa mfumo wa
ufunguzi na malipo ya mafao kupitia mtandao na huduma hii imeshaanza kwa baadhi
ya mikoa. Huduma hii inatoa fursa kwa wanachama walioko mbali na matawi yetu
kuweza kufungua madai mahali popote walipo, kufuatilia maendeleo ya ulipaji na
hatimaye kulipwa kwa mujibu wa kanuni za ulipaji wa mafao.
Kalimilwa alitumia nafasi hiyo
kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumshukuru kwa kuwajali wananchi
wake, kwa usikivu na juhudi kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na
Serikali yake ya awamu ya sita katika kuboresha maisha ya Watanzania.
Aidha, alimpongeza na kumshukuru kwa namna
anavyoendelea kutoa kipaumbele katika uwekaji mazingira wezesheji kwa
wawekezaji wa miradi mikubwa ambayo imeongeza ajira na hivyo kuongeza wanachama
na wachangiaji katika mfuko.
“Kwa upande wa masuala ya afya,
Serikali ya awamu ya sita imeboresha sana eneo hili kwa kujenga Hospitali na
vituo vingi vya afya na kuongeza vifaa tiba na Watumishi, juhudi ambazo
zimeleta tija kubwa kwa wanachama wetu na familia zao kupata huduma bora za
mafao ya matibabu,” alisema Kalimilwa.
Katika hatua nyingine kwa niaba
ya Bodi ya wadhamini, aliwashukuru na kuwapongeza watumishi wote wa mfuko kwa
juhudi kubwa za pamoja wanazozifanya katika kuwahudumia wanachama wao na kuwa
mfuko unatambua mchango wao katika kutekeleza majukumu waliyonayo.
Kalimilwa
alisema mfuko umeboresha mfumo wa Sekta isiyo rasmi mahsusi kwa wanachama wote
waliojiajiri, na umeandaa skimu maalum kwa wafanyakazi walio katika sekta rasmi
ili kuweza kujichangia kwa hiari kupitia skimu hiyo.
Alisema
pamoja na mambo mengine, Skimu hizo mbili (NISS na SS) zinalenga kupanua wigo
wa huduma za hifadhi ya jamii nchini na hivyo kuchangia katika kuondoa umaskini
kwa watanzania walio wengi na kuwa mfuko unaendelea kuweka mikakati ya kutosha
ili kuhakikisha kwamba watanzania wengi wanajiunga kwenye skimu hizo.
Aidha, Kalimilwa
alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha waajiri kutekeleza jukumu lao la kulipa
michango ya kwenye mfuko kwa wakati na kwa mujibu wa sheria na kueleza kuwa
jambo hilo ni muhimu sana kwa vile michango hiyo ikilipwa kwa wakati itaondoa
kero ya ufuatiliaji wa mafao kwa wanachama.
Alisema
kupitia mikakati hiyo, mfuko utaendelea kuishi kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “Huduma
Bora Popote Ulipo” na kuwa sasa ni mwaka wa tatu wamekuwa wakishiriki kusherehekea
maadhimisho hayo ya wiki ya huduma kwa wateja.
Afisa wa NSSF Mkoa wa Singida, Keneth Kalinjuma, alisema hivi sasa Mfuko huo umepanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa kuyafikia makundi yote ya wananchi waliojiajiri, kama waendesha bodaboda, bajaj, mama na baba lishe, wakulima na wafugaji ambao wanafika kujiandisha kwa ajili ya kuweka akiba zao ambazo zitakuja kuwasaidia baadae.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa (kushoto), akisoma hutuba ya maadhimisho hayo.
Mwanachama wa mfuko huo, Twaha Mwiru (kulia) akimlisha keke Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa.
Afisa wa NSSF Mkoa wa Singida, Keneth Kalinjuma, akizungumzia maboresho makubwa yaliyofanywa na mfuko huo ambapo sasa makundi mbalimbali ya wananchi waliojiajiri yanaweza kuweka akiba yao NSSF.
Afisa Matekelezo kutoak Mfuko wa Jamii wa PSSSF Mkoa wa Singida akipongeza maboresho makubwa yaliyofanywa na Mfuko wa NSSF.
Wageni waalikwa wakiwa kwenye hafla hiyo.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa. akimlisha keki mwanachama wa Mfuko huo, Hashimu Ramadhani.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa. akimlisha keki Mfanyakazi wa NSSF Mkoa wa Singida.
Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa, akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa mfuko huo, wanachama na wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo.
0 Comments