SACP Dkt. Debora Magiligimba
..............................................
RAIS wa Shirikisho la Polisi Wanawake Duniani - International Association
of Women Police (IAWP), Julia Jaegar, amemteua Kamishna wa Polisi kutoka
Tanzania, SACP Dkt. Debora Magiligimba, kuwa mjumbe katika Kamati ya Fedha ya
IAWP.
Hii ni heshima kubwa kwa SACP Dkt. Magiligimba, ambaye sasa atawakilisha
Tanzania katika kamati muhimu inayoshughulikia masuala ya kifedha ya IAWP
inayolenga kukuza haki, usawa, na maendeleo ya wanawake katika huduma za polisi
duniani kote.
Uteuzi wake ni ishara ya imani kubwa kwa uwezo wake katika kuleta maendeleo
ya kiutawala na kifedha katika IAWP.
Kamati ya Fedha ina jukumu la kuhakikisha rasilimali za shirika zinatumika
vyema katika kukuza malengo ya IAWP ya kuwasaidia wanawake polisi na kuboresha
huduma za polisi duniani.
SACP Dkt. Magiligimba anajiunga na mjumbe mwingine aliyeteuliwa kutoka Ujerumani katika kamati
hii, ambayo ni sehemu muhimu ya usimamizi wa kifedha wa IAWP.
Uteuzi huu unatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kuongeza
ufanisi wa IAWP katika masuala ya kifedha na utawala.
IAWP inatoa jukwaa la wanawake polisi ili kushirikiana, kubadilishana
uzoefu, na kusaidiana katika maeneo ya uongozi, mafunzo, na changamoto
zinazokumba wanawake katika tasnia ya polisi.
Mbali na uteuzi huu, SACP Dkt. Magiligimba pia alikuwa Mratibu wa Kanda ya
21 wa IAWP (Shirikisho la Kimataifa la Polisi Wanawake), ambapo aliongoza na
kuratibu shughuli za polisi wanawake katika nchi 11 za Kusini mwa Afrika. Nchi
hizo ni: Tanzania, Angola, Botswana, Eswatini, Lesotho, Malawi, Zimbabwe,
Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, na Zambia.
Katika nafasi hiyo, alifanya kazi ya kuhamasisha ushirikiano kati ya polisi
wanawake katika nchi hizo, na pia alishirikiana kupigania haki za wanawake, na
masuala ya kijinsia katika utekelezaji wa sheria na kuhamasisha polisi wanawake wa nchi hizo
11 kujiunga na IAWP.


0 Comments