Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

Header Ads Widget

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA UKIMWI YAPONGEZA UTEKELEZAJI WA AFUA ZA UKIMWI NJOMBE

NA. MWANDISHI WETU – LUDEWA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mheshimiwa Dkt. Elibariki Kingu ametoa pongezi kwa Mkoa wa Njombe kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu pamoja na TACAIDS kwa kuhakikisha watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI kuwawezesha kushiriki shughuli za kiuchumi.

Ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya Kamati hiyo leo tarehe 10 Januari, 2025 ilipotembelea kikundi cha kijamii cha watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI "Tujipime Labour Based Contractors", kilichopo kijiji cha Mundindi kata ya Mundindi wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Kamati hiyo imetembelea kikundi hicho kwa lengo la kujionea kazi mbalimbali zinazotekelezwa na wanakikundi, ikiwemo shughuli za ujenzi wa daraja moja “Vented Drift” katika barabara ya kutoka Mundindi hadi Mgogomo yenye urefu wa kilomita tano, na umetekelezwa kwa asilimia mia moja.

Aidha, majukumu mengine ya kikundi hicho ni kilimo pamoja na ufugaji wa nyuki.

Pamoja na hayo, Dkt. Kingu ametoa pongezi kwa wanakikundi kwa kutoogopa unyanyapaa wa kila aina na kuamua kuungana katika kikundi na kufanya kazi za maendeleo zinazowainua kiuchumi.

Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga, ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwathamini wananchi wa Ludewa kwa kuwaletea miradi mingi ikiwemo utoaji wa ajira kwa watu wa kila aina wakiwemo watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

Aidha amewasisitiza akina mama wajawazito kwenda kupima mapema ili kujua Afya zao, kwani kwa kujitambua mapema kama umepata maambukizi ya VVU husaidia kuanza dawa mapema, na kupunguza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Akiongea kwa niaba ya wanakikundi cha TUJIPIME, Mwenyekiti wa konga wilaya ya Ludewa, ndugu Marianus Mkinga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwakumbuka wananchi wa Ludewa wasioishi na wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kuwapa ajira na kujikwamua kiuchumi.

Post a Comment

0 Comments