..............................................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri
Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaki Rashidi Mchinjita, ameeleza kuwa baraza
kivuli litatumia mwaka 2025 kusimamia haki za wananchi, uwajibikaji wa Serikali
na kupigania mageuzi ya kweli ya kidemokrasia. Mchinjita amesema mwaka 2024
ulikuwa wa mateso makubwa hasa kutokana na migogoro ya ardhi, kasi ya kukua kwa
deni la serikali, hali mbaya ya kiuchumi, kuongezeka kwa matukio ya utekaji na
mauaji, maafa ya mvua za Elnino na kushindwa kwa serikali kutoa huduma bora kwa
wananchi. Ameeleza kuwa mwaka 2025 haupaswi kuendelea kutoa mateso tena.
Katika
kusisitiza msimamo huo, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kushirikiana na ACT
Wazalendo kufanya maamuzi yatakayoleta mabadiliko katika kuimarisha maisha yao
na kujenga taifa la wote.
Kauli hiyo ameitoa Januari 8, 2025
wakati akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama, Magomeni, Dar
es Salaam alipokuwa akitoa tathmini ya mwaka 2024 na kuelezea mwelekeo wa
Baraza hilo kwa mwaka 2025.
"Mwaka 2025 ni mwaka wa
Uchaguzi Mkuu ni mwaka wa uamuzi. ACT Wazalendo tumejizatiti kuimarisha haki za
kijamii, kupigania mageuzi ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi kwa maslahi
ya wote."
Aidha, Waziri Mkuu Kivuli amesema
mwaka 2024 ulikuwa na changamoto ya hali mbaya ya kiuchumi, ambapo deni la
serikali lilishuhudia kupaa na kufikia shilingi trilioni 93.7. Hali ambayo
imeathiri uwezo wa serikali kutoa huduma bora na kuajiri watumishi wa kutosha
katika sekta muhimu kama afya na elimu. Pia, tatizo la vijana kukosa ajira
limechangia ugumu wa maisha.
Kwa upande mwingine, amesema kuwa
moja ya changamoto kubwa zilizoathiri Watanzania mwaka 2024 ni migogoro ya
ardhi, ambayo imesababisha maumivu makubwa kwa wananchi wanyonge.
“Tangu kuingia madarakani Rais Samia Suluhu Hassan
kumeibuka kwa kasi ya ajabu ya wimbi la uporaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali
nchini. Wimbi hili limeenda sambamba na ukatili uliopindukia wa kupora mali,
mauaji ya raia, matumizi ya nguvu kuhamisha wananchi katika maeneo yao na
kusogeza mipaka ya hifadhi kwenye mipaka ya vijiji.” alisema Mchinjita.
Kuhusu hali ya huduma za kijamii,
Waziri Mkuu Kivuli ameonesha kusikitishwa na gharama kubwa za matibabu na mfumo
wa bima ya afya usio na usawa. Alisisitiza umuhimu wa kuwaunganisha wananchi
katika mfumo wa hifadhi ya jamii kutoa uhakika na kuzingatia mahitaji ya
wananchi wote bila kujali uwezo wao wa kifedha. “Ni jambo la aibu kuona
wananchi wa kipato cha chini wakinyimwa huduma za afya kwa sababu hawawezi
kumudu gharama. Afya ni haki, si bidhaa,” aliongeza.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu
Kivuli alilaani ongezeko la matukio ya utekaji, kupotea, na mauaji ya raia
wasio na hatia nchini huku Jeshi la Polisi likiwa kimya bila kuchukua hatua
madhubuti. Ameongeza kuwa watuhumiwa wakubwa wa vitendo hivyo ni vyombo vya
ulinzi na usalama hasa Idara ya usalama wa taifa na Jeshi la Polisi.
Akizungumzia demokrasia, Waziri
Mkuu Kivuli alisisitiza hitaji la kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, akibainisha
kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 umeonesha sura halisi ya Rais
Samia kuwa hataki mageuzi, kauli za R4 ni hadaa. “Ili tuwe na uchaguzi wa haki
na uwazi mwaka 2025, ni lazima tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi itakayohakikisha
kila kura ya Mtanzania inaheshimiwa,” aliongeza.
Amehitimisha kwa kuahidi kuwa Baraza Kivuli litaendelea kuwa sauti ya wananchi, huku ikisisitiza mshikamano wa kitaifa kupambana na changamoto zilizopo. Huu ni mwaka wa kuchukua hatua thabiti. Tanzania inastahili zaidi ya haya tunayoshuhudia sasa. Ni wakati wa kuleta mageuzi ya kweli.
0 Comments