Random Posts

𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐘𝐀𝐅𝐈𝐊𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐔𝐌𝐄𝐌𝐄 𝐊𝐀𝐓𝐈𝐊𝐀 𝐌𝐀𝐄𝐍𝐄𝐎 𝟓𝟖𝟐 𝐘𝐀 𝐖𝐀𝐂𝐇𝐈𝐌𝐁𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀𝐃𝐎𝐆𝐎, 𝐊𝐈𝐋𝐈𝐌𝐎 𝐍𝐀 𝐕𝐈𝐖𝐀𝐍𝐃𝐀 𝐓𝐀𝐍𝐙𝐀𝐍𝐈𝐀 𝐁𝐀𝐑𝐀

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetekeleza Mradi wa Usambazaji Umeme katika maeneo 582 ya wachimbaji wadogo, kilimo na viwanda Tanzania Bara, kwa gharama ya Shilingi bilioni 115.

Mhe. Makamba ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mhe. Mwanahamisi Athumani, Mbunge wa Viti Maalumu, aliyetaka kujua ni lini Serikali itatekeleza Mpango Mkakati Maalumu wa kuhakikisha maeneo ya wachimbaji wadogo yanafikishiwa umeme wa kutosha kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji.

Akijibu swali hilo, Mhe. Makamba amesema kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Aprili, 2023 na kwa sasa umefikia hatua za mwisho za utekelezaji.

Aidha, amesema Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Madini inaendelea kuainisha maeneo ya kipaumbele yatakayofikishiwa huduma ya umeme katika hatua zinazofuata, kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.

Sambamba na hilo, Mhe. Makamba amesema Serikali kupitia TANESCO, kwa kutumia fedha za ndani, inaendelea kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme pamoja na ujenzi na uboreshaji wa vituo vya kupoza umeme katika mikoa mbalimbali nchini, hususan maeneo yenye changamoto ya low voltage.

Amesema hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha maeneo yote ya uzalishaji yanafikiwa na huduma ya umeme ya kutosha na ya uhakika.

Mhe. Makamba amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wachimbaji wadogo, wakulima, viwanda na maeneo mengine ya uzalishaji yanapata umeme wa kutosha na wa uhakika wakati wote, ili kupunguza gharama za uzalishaji, kuongeza tija na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini.

Post a Comment

0 Comments