.........................................
Na Denis Chambi, Tanga.
KUTOKANA na kasi ya ukuaji na maendeleo ya mkoa wa Tanga inayotokana na uwekezaji wa Serikali kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo Bomba la Mafuta ghafi pamoja na uboreshaji wa Bandari Shirika la Nyumba Tanzania 'NHC' linaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za Makazi pamoja na biashara ili kuweza kukidhi ongezeko la watu na uhitaji.
Akizungumza ofisni kwake Meneja wa Shirika la Nyumba Tanzania 'NHC' Mkoa wa Tanga Mhandishi Mussa Kamendu amesema kuwa kumekuwa na ongezeko wa watu wakiwemo watumishi wa umma , taasisi na sekta binafsi hali ambayo inaonyesha kuwepo na uhitaji wa Makazi pamoja na nyumba za biashara kadiri miaka inavyokwenda hii ikichangiwa zaidi na kasi ya maendeleo ya mkoa huo ambao unazidi kukua kiuchumi.
"Tumekuwa tukitekeleza miradi kadhaa ambayo ni sehemu ya kukabliana na ongezeko la watu kwa maana ya mahitaji ya nyumba, tunafanya miradi hiyo kutokana na mabadiliko maendeleo na fursa mbalimbali ambazo zipo katika mkoa wa Tanga kwa sasa"
"Tunazo nyumba 20 za Makazi ambazo tumeshaziuza mradi huu upo hatua ya mwisho tunategemea utakamilika mwanzoni mwa mwaka ujao wa fedha tunazo nyumba nyingine ambazo zina sehemu za ofisi , Benki pamoja na biashara"amesema Kamendu.
Amesema kwa sasa Shirika hilo lina zaidi ya wapangaji 900 lakini kutokana na kuwa ujio wa mradi wa Bomba la Mafuta ghafi linalotoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga Tanzania umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watu hususani kutoka nje ya nchi.
"Kutokana na maendeleo Mkoa wa Tanga kuna watu wengi wanaamua kuhamia mkoa wa Tanga kwa sababu ya fursa zilizopo kwa sasa ambao wote hawa wanahitaji nyumba kwa sababu hiyo sisi kama Shirika tumeendelea kujipanga" amesema.
Aidha Kamendu ameongeza kuwa pamoja na ujenzi wa makazi hayo Shirika hilo linaendelea kuboresha na kukarabati nyumba zake zote zinazoendelea kutumiwa na wapangaji kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma.
"Nyumba pia zilizopo tunafanya juhudi ya kuzikarabati kwa lengo la kufanya nyumba za wapangaji wetu ziweze kuwa katika hali bora na bado tunaendelea na zoezi hilo la kukarabati ambao unahusisha kupaka rangi, kubadilisha mifumo ya umeme na maji " amesema Mhandishi Kamendu.
Kauli mbiu ya Serikali ya mkoa wa Tanga chini ya Mkuu wa mkoa huo Balozi Dkt Batilda Buriani isemayo "Tanga lango kuu la uchumi Afrika Mashariki na SADC' inaonyesha Tanga kuwa miongoni mwa Mikoa hapa nchini inayotazamwa na kuwavutia wawekezaji wa kutoka ndani na nje ya nchi.

0 Comments