Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza wakati alipozindua Miongozo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi Miongozo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwenye ukumbi wa Msekwa , bungeni mjini Dodoma Septemba 14, 2016.
.......................................................................
Na Eleuteri Mangi na Beatrice Lyimo, MAELEZO, Dodoma.
Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa Mfumo wa Anwani za
Makazi na Postikodi una manufaa mengi ambao utarahisisha ukusanyaji wa mapato
kutoka vyanzo mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa
amesema hayo leo mjini Dodoma wakati alipokuwa akizindua Mwongozo wa Mfumo wa
Anwani za Makazi na Mwongozo wa Postikodi ambao utatumika nchi nzima.
“Kama kila mlipa kodi tutamfahamu
kwa uhakika anaishi wapi, tutamutoza kodi stahiki na hili ni jambo
muhimu la utawala bora” amefafanua Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa
amesema kuwa uwepo wa anwani ya makazi nchini utasaidia kurahisisha ukusanyaji
wa mapato mbalimbali ikiwa ni jukumu muhimu la utawala bora.
Aidha, amesema kuwa mfumo
huo wa anwani za makazi utaiwezesha Serikali kuwahudumia wananchi wake kirahisi
ikiwa ni pamoja na kutoa ulinzi, kurahisisha mawasiliano miongoni mwa wananchi
na Serikali.
Vile vile mfumo huo
utasaidia kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma za kijamii,
huduma za kibiashara, huduma za dharura na uokoaji, kurahisisha sensa,
kuboresha daftari la wapiga kura, kuboresha huduma za posta na kuwezesha utoaji
wa biashara mtandao.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika nchi nyingi za viwanda na nchi zilizoendelea suala
la miundombinu ikiwemo Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi ni muhimu na
linaeleweka kwa kila mtu katika kuanzisha, kukuza na kuendeleza uchumi wa
viwanda.
“Kwa kutumia mfumo huu,
viwanda viwe vikubwa au vidogo vinatambulika viko wapi kwa anwani zao za makazi
na hivyo kuweza kupima kirahisi ukuaji
wa viwanda” alifafanua Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amesisitiza taasisi zote za umma na zile za binafsi zianze
kutumia anwani za makazi na postikodi ili kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi
ikiwa ni pamoja na kutumia katika makusanyo ya mapato.
Waziri Mkuu Majaliwa amewasisistiza
wadau wote nchini kuzingatia kuwa na anwani ni haki ya kila mtu na pia kupata
huduma za msingi kupitia mfumo huo ni haki ya kila mtu.
Aidha, dhana ya kuwa “dunia
ni kijiji” inapaswa kuwa chachu ya kupata huduma zote mahali ulipo, inahitaji juhudi
za makusudi za kuhakikisha Tanzania imekuwa sehemu ya kijiji hicho na inakuwa
ni moja ya mataifa kinara wa kutoa huduma mbalimbali kwa ufanisi kwa kutumia
Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi.
Kwa upande wake Balozi
wa Anwani za Makazi Duniani Prof. Anna Tibaijuka amesema kuwa anajivunia mradi
huo kutekelezwa nchini ambao utasaidia kuonesha watu mahali wanapoishi ambapo Tanzania
imefanikiwa kuwa na anwani za makazi nchi nzima licha ya changamoto ya kuwa na miji mingi ambayo haijapangwa.
Zao la anwani za
makazi linatokana na Umoja wa Posta Dunia (UPU) iliyopitishwa katika mkutano mkuu
wa 25 uliofanyika mjini Doha, Qatar mwaka 2012 ambao ulipitisha azimio la
kuzitaka nchi zote duniani kuhakikisha kuwa kila mtu anakuwa na anwani.
0 Comments