WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itapitia upya sababu
za kuanzishwa kwa Mamlaka ya Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) kufuatia mamlaka hiyo
kuendeshwa kwa ubabaishaji.
Hatua hiyo imekuja baada ya mamlaka hiyo kushindwa kusimamia
uendelezaji wa bonde hilo na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Septemba 26,
2016) wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Ikwiriri
mkoani Pwani.
Alisema baada ya mapitio hayo shughuli za mamlaka hiyo
zitahamishiwa kwenye mamlaka nyingine za serikali kwani
RUBADA imeshindwa kufanyakazi hiyo kwa muda mrefu.
“RUBADA wamepewa ardhi lakini wameshindwa kuiendeleza, tutafanya
upya mapitio ya kuanzishwa kwake,” alisema.
Akizungumzia kuhusu Kampuni ya Agro Forestry Plantation inayotaka
kujenga kiwanda cha sukari wiyani Rufiji aliitaka kampuni hiyo kuhakikisha
asilimia 60 ya watumishi watakaowaajiri wawe ni vijana wa wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alimuagiza
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi, kwenda wilayani
Rufiji kutatua mgogoro wa mpaka kati ya Wilaya ya Mkuranga na Ikwiriri.
Waziri Mkuu amelitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka
kwa wananchi wa Ikwiriri kuhusu kutotatuliwa kwa mgogoro huo uliodumu kwa muda
mrefu.
Naye Mkurugenzi wa halshauri ya wilaya hiyo, Rashidi Salum
alimweleza Waziri Mkuu kuwa, mgogoro huo umeshatatuliwa kwa ngazi ya
wilaya hivyo hatua iliyosalia ni kwa uWaziri wa Ardhi kufika na
ramani ili kutoa uamuzi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 27, 2016

0 Comments