WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameahidi kukutana na wafanyabiashara wa soko
la Sabasaba mkoani Dodoma ili kuzungumzia namna ya kulikarabati na kulifanya
liwe la kisasa.
Amesema miongoni mwa mambo watakayoyajadili katika kikao hicho ambacho
hakutaja siku ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara hasa kwa
wanaouza bidhaa nje ya maduka.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Oktoba 5, 2016) wakati
alipotembelea maduka hayo yaliyoko katika barabara ya One Way inayopita
katikati ya barabara ya sita hadi ya 11 pamoja na soko la Sabasaba akiwa kwenye
ziara ya kukagua maeneo ya kutolea huduma za jamii mjini Dodoma.
Amesema Serikali tayari imeshahamia Dodoma hivyo wafanyabiashara wanatakiwa
kutumia fursa hiyo kwa kuboresha biashara zao ili waweze kumudu ushindani wa
soko.
“Wafanyabiashara lazima mboreshe biashara zenu, muongeze usafi zaidi na
ikiwezekana muimarishe majengo yenu yawe ya kisasa zaidi kwani haiwezekani
maduka ya Makao Makuu ya Nchi yawe katika hali hii,” amesema.
Pia Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara hao wasiogope kwenda kukopa
katika taasisi mbalimbali za kifedha kwa lengo la kujiongeza mitaji na
kupanua biashara.
Amesema tayari alishatoa maagizo kwa wamiliki wa benki kuhakikisha
wanawawezesha wajasiriamali wadogo kwa kuwapa mikopo, hivyo aliwataka wasiogope
na badala yake wachangamkie fursa hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATANO, OKTOBA 05, 2016

0 Comments