Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu anapenda
kutoa ufafanuzi kuhusu Tamko la Shirikisho la Watu
Wenye Ulemavu nchini (SHIVYAWATA) kuhusu makundi ya wananchi wanaostahili
kupata msamaha wa matibabu. Aidha, baadhi ya Vyombo vya habari vimenukuu
maelezo ambayo yametolewa na mwenyekiti wa SHIVYAWATA kuhusu
Makundi yanayostahili kupata msamaha wa Matibabu nchini.
Kutokana na Maelezo hayo, napenda kutoa ufafanuzi ufuatao; Sera ya Afya ya Mwaka (2007) inatambua kuwa wapo wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuzifikia huduma za Afya wakiwemo watu Wenye Ulemavu. Aidha, Kwa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na.9/2010 ambayo, pamoja na mambo mengine, Sheria inabainisha kuwa Watu Wenye Ulemavu wana haki ya kuondolewa vikwazo katika kupata huduma za Afya.
Kwa kuzingatia maelekezo ya Sera ya Afya (2007) na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu(2010) Wizara yangu inatambua na itaendelea kuhakikisha kwamba Watu Wenye Ulemavu Wasio na Uwezo wa kugharamia huduma za Matibabu wanapatiwa Msamaha wa Matibabu katika Ngazi zote kuanzia Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Mikoa na Hosptali za Rufaa. Pia kwa kutambua umuhimu wa huduma ya Afya kwa Wananchi wote, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika mchakato wa kutungwa kwa sheria itakayowezesha wananchi wote wakiwemo Watu Wenye Ulemavu kupata Kitambulisho cha Bima ya Afya. Hatua hii itawaondolea vikwazo, wananchi wote wakiwemo watu Wenye Ulemavu katika kuzifikia huduma za Afya pasipo kikwazo cha ukosefu wa fedha.
Naomba kuchukua fursa hii kuwahakikishia ndugu zangu Wenye Ulemavu kuwa wanayo haki ya kupata huduma za matibabu katika ngazi zote. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia na kuhakikisha makundi maalum wakiwemo watu Wenye Ulemavu ambao hawana uwezo wa kuchangia huduma za Matibabu wanapata msamaha wa matibabu katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Natoa
maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwatambua Watu Wenye Ulemavu Wasio
na Uwezo wa kuchangia huduma za matibabu na kuimarisha Kitengo cha Huduma za Ustawi
wa Jamii katika vituo vya kutolea huduma za Afya ili viweze
kuwatambua na kutoa msamaha kwa watu wenye ulemavu wasio na uwezo
ili waweze kupatiwa matibabu bila ya vikwazo vya ukosefu wa fedha.
Aidha,
ni marufuku kwa Mtumishi yeyote wa Sekta ya Afya kuonesha vitendo vyovyote vya
unyanyapaa na unyanyasaji kwa Watu Wenye Ulemavu wanaofika katika vituo vya
kutolea huduma za afya. Mtumishi atayethibitika kuonesha kwenda kinyume
cha maadili ya utumishi wa umma na taaluma za Afya kwa kufanya vitendo vya vya
unyanyapaa na unyanyasaji kwa makundi maaalum ikiwemo watu wenye
ulemavu atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
Wizara yangu inafanya jitihada kuhakikisha kuwa inaondoa vikwazo vyote vinavyowanyima watu wenye ulemavu kupata huduma za afya wanazohitaji ikiwemo kuhakikisha kuna mazingira mazuri yanayowawezesha kufika hospitali kwa kuweka miundo mbinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Vile vile, ninawataka watoa huduma wote kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu wanapofika hospitali. Wapatiwe huduma haraka ili kuwapunguzia usumbufu kutokana na mahitaji yao ya kimwili. Kama ambavyo tumefanya kwa Wazee niwaagiza kila kiongozi ahakikishe anaweka utaratibu mzuri wa kuwapa nafasi ya kwanza watu wenye ulemavu tukijifunza kwa jinsi tulivyofanya na kufanikiwa katika eneo la kuhudumia wazee.
Watu wenye ulemavu ni wenzetu, watoto wetu, ndugu na jamaa zetu. Tuwahudumie kwa upendo na kuhakikisha wanapata fursa sawa na wengine
Imetolewa
na
MHE. UMMY A. MWALIMU (Mb.)
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto
15/10/2016

0 Comments