STRAIKA kinda anayechipukia kwa kasi katika timu ya Azam
FC, Shaaban Idd, ameeleza siri ya mafanikio yake ya hivi karibuni, akidai kuwa kitendo
cha Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, kumuondolea uoga na kumpa maelekezo bora ndio
mambo makuu yanayombeba hivi sasa.
Kinda huyo aliyelelewa kwenye kituo cha Azam FC
Academy, jana alifunga mabao mawili muhimu na kutengeneza moja kwenye ushindi
mnono wa Azam FC wa mabao 4-1, wakiifunga Mwadui ya Shinyanga, mengine
yakifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’ na Francisco Zekumbawira.
Mabao hayo yamemfanya Idd kutimiza mabao matatu msimu
aliyoifungia Azam FC baada ya kupandishwa kwenye kikosi cha timu kubwa huku
akitoa pasi mbili za mabao, moja akimpa nahodha Bocco kwenye ushindi wa mabao
3-2 dhidi ya Kagera Sugar na nyingine akiitoa jana kwa straika nyota kutoka
Zimbabwe, Zekumbawira.
Idd ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa mbali na kocha wa timu
hiyo kumuondolea uoga, pia maelekezo mazuri anayompa na kumpa uhuru uwanjani
nayo yamechangia kubadilika kwa kiwango chake kwenye mechi za hivi karibuni
tofauti na mechi za awali mwanzoni mwa msimu.
“Kitu cha kwanza napenda kumshukuru Mwenyenzi Mungu
kwa kuweza kunijalia kuweza kuisaidia timu yangu kuibuka na ushindi wa mabao
4-1, pia napenda kumshukuru kocha wangu kwa kunipatia maelekezo mazuri ya
kunifundisha jinsi mpira unavyochezwa na mimi bila kipingamizi nimetendea haki
maelekezo yake na kuweza kuisaidia timu yangu kuibuka na ushindi.
“Kwa kweli ninafuraha sana na hii pia ni siku muhimu
kwa ajili ya kiongozi wetu mkubwa ambaye amefariki (Mzee Said Mohamed Abeid)
hivi majuzi (Jumatatu iliyopita), hivyo ushindi huu una maana nyingi sana
kwetu,” alisema.
Kocha
ampa uhuru
Idd aliyeibuka mfungaji bora wa michuano ya Azam Youth
Cup yaliyofanyika mwaka huu akifunga mabao matano, alisema kuwa katika vitu
vilivyomsaidia kubadilika hivi sasa ni kutokana na kocha kumpa zaidi uhuru uwanjani.
“Kocha kanipa nafasi na kanipa uhuru wa kujiamini
nisiwe na uoga wowote tofauti na nilivyokuwa nikicheza mwanzo kwani nilikuwa
nacheza na uoga, hivyo kocha kaliangalia hilo na kulitambua na hatimaye akanipa
nafasi na kuniambia nicheze nisiwe na uoga wowote, nisiogope kitu chochote na
nicheze kwa kiwango change,” alisema.
Alisema kwa kuwa ligi ya msimu huu ni ngumu na huu
ukiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza, amesema atazidi kupambana na kujitahidi kuweza
kuisaidia zaidi timu yake hiyo katika mzunguko wa pili wa ligi unaokuja na
michuano mingine pamoja na yeye kujijengea uzoefu.
Mashabiki
nao wamuamini
Straika huyo, 18, alichukua fursa hiyo kuwaomba
mashabiki wa Azam FC waendelea kumuunga mkono, kumvumilia na kumuamini zaidi kwani
bado ana mambo mengi anayotaka kuifanyia Azam FC.
“Mashabiki wasichoke kutuombea dua na kutusapoti
katika hii kazi yetu tunawaahidi tutawapa burudani nzuri na timu yetu kuwa
katika nafasi nzuri kwenye mzunguko wa pili,” alimalizia kinda huyo.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola ambacho
ni mahususi kabisa kwa ajili ya kuchangamsha mwili wako na kuburudisha koo lako
pamoja na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, imemaliza
mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo
ikijikusanyia jumla ya pointi 25 ikizidiwa pointi 10 tu na vinara Simba
waliojizolea 35.
0 Comments