KOCHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na
Kati Azam FC, Yeray Romero, amesema kuwa ushindi wa mabao 4-1 walioupata dhidi
ya Mwadui jana ni muhimu kwa kikosi hicho, akidai ni zawadi tosha ya kumuenzi aliyekuwa
mwenyekiti wa timu hiyo, Mzee Said Mohamed Abeid, aliyefariki dunia Jumatatu
iliyopita jioni.
Mabao ya Azam FC yalifungwa na nahodha John Bocco ‘Adebayor’,
Shaaban Idd aliyefunga mawili na Francisco Zekumbawira, huku lile la Mwadui
likiwekwa nyavuni na Hassan Kabunda.
Yeray ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa wameondokewa na mtu
muhimu kwenye klabu, hivyo ushindi huo unawafanya kujumuika naye pamoja katika
kumuenzi.
“Ushindi tulioupata ni mkubwa, kilichotokea ni
wachezaji wamejaribu kuona yale madhaifu yaliyotokea na wameyafanyia kazi kwani
tuliweza kutanguliwa kufungwa bao lakini wachezaji wakaja juu na kupambana na
mabadiliko tuliyofanya kipindi cha pili yaliweza kutupa ushindi huo mnono.
“Kiufupi kipindi cha kwanza kulikuwa na mapungufu
yaliyoonekana, kipindi cha pili sisi walimu tulikitumia kurekebisha tuliweza
kumuingiza Shaaban (Idd) na Francisco (Zekumbawira) lakini pia Singano
(Ramadhan) alitangulia kuingia, tatizo lililoonekana kipindi cha kwanza ni
umaliziaji lakini mabadiliko hayo yaliweza kuufanya mchezo kuwa rahisi kwetu na
kupata mabao hayo,” alisema.
Ushindi huo umewafanya mabingwa hao kutimiza jumla ya
25 na kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL)
ikiwa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo.













0 Comments