Mwenyekiti wa wa
kijiji cha Mngazi, mkoani Morogoro akitoa maoni kwa niaba ya wananchi wa kijiji
hicho kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin
Ngonyani, wakati alipokagua barabara ya Morogoro- Kisaki (KM 133) ambayo
inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani (Mwenye Miwani),
akifafanua jambo kwa wananchi wa kijiji cha Mngazi mkoani Morogoro, wakati
alipokagua barabara ya Morogoro- Kisaki (KM 133) ambayo inatarajiwa kujengwa
kwa kiwango cha lami.
Muonekano wa Daraja la
Ruvu lililopo katika barabara ya Morogoro –Kisaki (KM 133), ambapo barabara
hiyo inatarajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.
Picha na Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
................................................................................................................
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani amesema kuwa serikali
itajenga barabara ya Morogoro hadi Kisaki KM 133 Kwa kiwango cha lami ili iweze
kupitika na wananchi kuweza kuitumia kipindi chote cha mwaka.
Mhandisi Ngonyani
amesema hayo mara baada ya kukagua barabara hiyo inayounganisha wilaya ya Morogoro
Mjini na Morogoro Vijijini ambambo amesisitiza kuwa barabara hiyo ni kiungo
muhimu kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani.
Amefafanua kuwa ujenzi wa barabara hiyo utaanzia Morogoro
Mjini hadi kijiji cha Mvuha (KM 78) Kwa lengo la kuunganisha Morogoro Mjini na
kituo cha treni ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kilichopo eneo la Kisaki na
hivyo kuongeza idadi ya wasafiri na shehena ya mizigo itakayotumia usafiri wa
treni hiyo.
“Tunatambua umuhimu wa
barabara hii kwa wananchi wa Morogoro na mikoa ya jirani na sasa tunaendelea na
mipango ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami ili iweze kupitika hata
vipindi vya masika”, amesisitiza Mhandisi Ngoyani.
Ameongeza kuwa
kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutachochea fursa za utalii katika
hifadhi ya Taifa ya Mikumi na Mbuga za Selous kwa kuunganisha na mikoa ya
Morogoro, Iringa na Mbeya na hivyo kukuza pato la Taifa kupitia utalii.
Mhandisi Ngonyani
ameeleza kuwa ujenzi huo utaanza kwa kujenga daraja jipya la Dutumi ambalo
limekuwa halipitiki wakati wa masika pamoja na kukarabati Daraja la Mto Mvua
ili liweze kuwa katika ubora unaostahili na kupitisha maji kwa urahisi bila kusababisha
madhara kwa wakazi wa eneo hilo.
Naye, Mhandisi Mkuu wa
Mkoa kutoka Wakala wa barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Godwin Andalwisye, amesema
kuwa hatua za awali za ujenzi wa daraja la Dutumi umeanza ambapo usanifu wa
kina umeshafanyika.
“Kwa sasa tumeshaandaa
michoro itakatumika katika ujenzi wa daraja hili, tutahakikisha ujenzi wake
unaanza na kukamilika kwa wakati ili kuimarisha sehemu hii na kupitika kwa
urahisi hata wakati wa masika”, amesisitiza Mhandisi Andalwisye.
Katika hatua nyingine
Mhandisi Ngonyani amemhimiza Mkandarasi wa GNMS anayejenga barabara ya Bigwa
(KM 2) kukamilisha ujenzi wake kwa kiwango cha lami ifikapo Januari mwakani.
Naibu Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano yupo Mkoani Morogoro katika ziara ya kukagua
Miundombinu ya barabara, Madaraja na Reli.
Imetolewa na kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.



0 Comments