Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Prof. Idrissa
Mshoro akiwasili katika viwanja vya chuo hicho kwa ajili ya kuhudhuria katika
mahafali ya 10 ya chuo hicho yaliyofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Mhe. Cleopa Msuya akimtunuku
mmoja wa wanafunzi wa shahada ya Udaktari wa Falsafa (PhD) aliyoipata katika
chuo hicho. Mahafali hayo yamefanyika jana Jijini Dar es Salaam katika viwanja
vya chuo hicho.
Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi, Mhe. Cleopa Msuya
(kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine waliohudhuria kwenye
mahafali ya 10 ya chuo hicho akiwemo Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la chuo hicho,
Prof, Evelyne Ambede (wa pili kushoto), wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella Manyanya. Mahafali hayo yamefanyika jana
Jijini Dar es Salaam katika viwanja vya chuo hicho.
Baadhi ya wanafunzi wa shahada na stashahada waliohitimu
katika chuo hicho wakiwa katika viwanja vya chuo. Mahafali hayo yamefanyika
jana jijini Dar es Salaam.
...................................................................
Na
Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Chuo
Kikuu Ardhi kimekamilisha ujenzi na uwekaji wa vifaa katika Bandari ya Tanga
ikiwa ni moja ya miradi ya kiutafiti inayofanywa chuoni hapo kwa ajili ya
kupima hali halisi ya bahari.
Makamu
wa Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idrissa Mshoro ameyasema hayo alipokuwa akisoma
hotuba wakati wa mahafali ya 10 ya chuo hicho yaliyofanyika jana chuoni hapo
jijini Dar es Salaam.
Prof.
Mshoro amesema kuwa pamoja na jukumu la kutoa wahitimu katika fani mbalimbali
kwa maendeleo ya nchi pia chuo hicho kina majukumu ya kufanya utafiti na kutoa
ushauri wa kitaalam hivyo kupitia Mradi wa Utafiti wa Mabadiliko ya Tabia Nchi
uliofadhiliwa na Serikali ya Norway kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania umeweza
kufanikisha ujenzi huo.
“Madhumuni
ya Mradi huu ni kusaidia kuboresha mawasiliano kati ya Bandari na watumiaji
wake kwani taarifa sahihi zitakazotolewa kuhusu hali halisi ya bahari
zitasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kutumia Bandari hiyo pia, taarifa hizo
zitakuwa msaada mkubwa kwa wadau wengine kama wavuvi, watalii pamoja na
watafiti mbalimbali,” alisema Prof. Mshoro.
Ameongeza
kuwa katika kutoa ushauri na huduma za kitaalam, chuo kimetekeleza miradi
mbalimbali ya Serikali, taasisi za Umma na Binafsi katika fani zote
zinazofundishwa chuoni hapo hivyo kusaidia katika kuongeza kipato cha chuo kwa
ajili ya miradi, kutoa motisha kwa wafanyakazi pamoja na kutoa fursa kwa wana
taaluma kupata uzoefu kwa vitendo katika fani mbalimbali walizosomea.
Aidha,
Prof. Mshoro ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuendelea kukipatia chuo
fedha na misaada mingine kwa ajili ya kuendeshea shughuli za chuo ambapo kwa
mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetengea jumla ya shilingi bilioni 5 kwa
ajili ya bajeti ya maendeleo ya chuo hicho.
Akiongelea
kuhusu wahitimu, Prof. Mshoro amefafanua
kuwa jumla ya wanafunzi 968 watatunukiwa shahada na stashahada mbalimbali
ambapo wanafunzi 868 watatunukiwa shahada za awali, 80 shahada za uzamili, 14
watatunukiwa stashahada pamoja na shahada za uzamivu kwa wanafunzi 6.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Stella
Manyanya amesema kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa wasichana kujiunga na
masomo ya sayansi kwani idadi imeonyesha kuwa wahitimu wa kike ni 320 ambayo ni
sawa na asilimia 33 ya wanafunzi wote hivyo ametoa rai kwa wasichana kutumia
fursa za kusomea masomo hayo bila kuogopa.
Mhandisi
Manyanya amewashauri vijana kujikita kusoma masomo yatakayowapelekea kujiajiri
wenyewe kuliko yale yanayohitaji kuajiriwa kwani njia hiyo itasaidia kujikwamua
kiuchumi kwa haraka na kuchangia katika maendeleo ya taifa.





0 Comments