BAADA ya kupona majeraha ya nyonga, beki wa kulia wa Klabu Bingwa ya
Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, amesema kuwa hivi
sasa anapambana vilivyo kurejesha makali yake yaliyomfanya akubalike na
mashabiki wa timu hiyo.
Category:
Team:
Azam FC
Beki huyo kipenzi wa mashabiki wengi wa soka nchini, amerejea
mazoezini hivi sasa kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara (VPL), alishindwa kuitumikia vema timu hiyo baada ya
kukosa mechi 10 za mwisho za mzunguko wa kwanza wa ligi kufuatia
majeraha hayo.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
Kapombe alisema kuwa kwa sasa anazidi kujiandaa vema kupitia mazoezi
wanayopewa na benchi la ufundi la timu hiyo pamoja na mengine binafsi
anayoyafanya peke yake.
“Mimi binafsi nimejiandaa vizuri na naendelea kujiandaa vizuri kwa
mazoezi ambayo tunapewa na mengine ya kwangu binafsi, yote hayo nafanya
ili kupambana na kurejesha makali yangu ili kuisaidia Azam FC,” alisema.
Kapombe alisema kwa sasa anaendelea vizuri na afya yake ipo vizuri
kabisa kuweza kupambana kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mzunguko wa
pili wa ligi unaoanza Jumamosi ya wikiendi hii.
Sura mpya dirisha dogo
Kapombe pia alifurahishwa na namna wachezaji wapya waliosajiliwa
kwenye dirisha dogo la usajili, ambapo amedai kuwa ni wachezaji wazuri
na anaamini ya kuwa wataisadia sana Azam FC kuelekea mechi za mzunguko
wa pili.
“Mpaka sasa kuna sura mpya ambazo zimeongezwa, ni wachezaji wazuri
wanaokuja kuziba mapungufu ambayo tumayaona mzunguko wa kwanza, kila
mchezaji aliyekuja hapa anasifa yake na uzuri wake kuweza kuisaidia timu
yetu katika kufikia malengo tuliyojiwekea,” alisema.
Hajawaacha mashabiki
Beki huyo mwenye sifa ya kupandisha mashambulizi kwa kasi na uwezo
kufunga mabao, aliyeweka nyavuni mabao 11 msimu uliopita, kuelekea
raundi ya pili ya ligi amewaachia ujumbe mashabiki wa timu hiyo
akiwaambia kuwa waunganishe nguvu kuwasapoti uwanjani katika mechi zao.
“Mimi ninachowaomba mashabiki wa Azam FC ni waendelee kuwa nasi
katika vipindi vyote vya shida na raha, waunganishe nguvu na waendelee
kutusapoti katika mechi za raundi ya pili ili na sisi tuweze kufika pale
Azam FC inapohitajika kufika,” alimalizia.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola,
kinachoburudisha koo na kuchangamsha mwili pamoja na Benki bora kwa
usalama wa fedha zako ya NMB, inatarajia kufungua ng’we ya mzunguko wa
pili kwa kukipiga na African Lyon Jumapili hii Desemba 18 kwenye Uwanja
wa Uhuru, Dar es Salaam saa 10.00 jioni.


0 Comments