Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya
misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti
uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine
katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio
makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Katika
kuelekea sikukuu za mwisho wa Mwaka, Krismas na mwaka mpya 2017 Jeshi la Polisi
Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kwa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo
yote. Katika kuhakikisha wakazi wa Mkoa wa Mbeya wanasherehekea kwa amani na
utulivu sikukuu ya mwaka mpya, tumeandaa mpango mkakati kama ifuatavyo:-
MPANGO MKAKATI WA JESHI LA POLISI MKOA
WA MBEYA KUELEKEA SIKUKUU YA NA MWAKA MPYA:
1. Ulinzi na usalama katika nyumba za
ibada
Kwa
makanisa ambayo yatakuwa na ibada za mkesha kwa siku ya tarehe 31.12.2016
kutakuwa na askari ambao wataimarisha ulinzi na usalama kwa kusaidiana na kamati
ya ulinzi na usalama ya kanisa/msikiti husika. Kuhakikisha ulinzi ndani na nje
ya kanisa/msikiti unakuwepo, ulinzi katika maeneo ya maegesho ya magari.
2. Kumbi za starehe
Jeshi
la Polisi linawataka wamiliki wa kumbi za starehe kufuata na kuzingatia taratibu
za uendeshaji biashara zao hasa kwa kuzingatia muda wa kufungua na kufunga
kumbi zao kulingana na vibali vya biashara zao, kuzingatia idadi ya watu wanaopaswa
kuingia ukumbini kulingana na ukubwa wa ukumbi ili kuepuka madhara yanayoweza
kujitokeza. Pia tunawataka kuweka walinzi wa ndani ya ukumbi na nje hasa maeneo
ya maegesho ya magari ili kudhibiti uhalifu na wahalifu.
3. Waendesha vyombo vya moto na
watumiaji wengine wa barabara.
Kutokana
na kuwepo ongezeko la vyombo vya moto katika Mkoa wa Mbeya magari, pikipiki na bajaji
kila mtumiaji wa vyombo hivi anatakiwa kuzingatia utimilifu wa afya yake,
usalama wa chombo chake pamoja na kuheshimu, kufuata na kuzingatia sheria na
alama za usalama barabarani. Aidha watembea kwa miguu kuhakikisha wanakuwa
waangalifu wakati wa kuvuka barabara ili kuepuka ajali. Jeshi la Polisi Mkoa wa
Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa vyombo vya moto
na watumiaji wengine wa barabara unakuwepo, pia kwa wageni wanaoingia na kupita
kuelekea nchi jirani na mikoa jirani wanapita bila usumbufu wowote.
4. Uangalizi wa watoto katika kipindi
chote cha sikukuu.
Jeshi
la Polisi Mkoa wa Mbeya linawataka wazazi na walezi kuhakikisha kila mmoja
anakuwa makini na mtoto wake kwa kutoa uangalizi katika kipindi chote cha
sikukuu ya mwaka mpya. Kuhakikisha watoto wanakuwa na waangalizi pindi
wanapotoka kwenda maeneo ya mbali kama vile sehemu za kuabudu makanisani na
misikitini, sehemu za michezo ya watoto ili kuepuka matukio ya kupotea kwa
watoto na hata kuepuka vitendo vya uhalifu dhidi ya watoto. Aidha ni wito wa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kila mzazi, mlezi na jamii kwa ujumla kuwa makini
na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pindi wanapoona mtoto/watoto waliopotea.
5. Ulinzi na usalama katika nyumba za
kuishi/makazi yetu
Pia
ulinzi na usalama ni muhimu katika makazi yetu, vikundi vya ulinzi shirikishi
vilivyopo katika mitaa vina kazi ya kufanya katika kipindi hiki kutokana na
ongezeko la watu. Aidha Jeshi la
Polisi litakuwa pamoja na vikundi hivi kufanya doria ya pamoja katika maeneo
tete na makazi. Pia ni rai yangu kwa kila mmoja kuhakikisha anapotoka anaacha
mtu/muangalizi ili kuepuka vitendo vya uvamizi, uvunjaji.
WITO WA KAMANDA.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya kwa
ujumla kuwa watulivu, kusherehekea kwa utulivu na amani sikukuu ya mwaka mpya
2017. Aidha anatoa wito kwa wananchi kuacha kuzurura ovyo na pia kushirikiana
na vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu
katika maeneo yao.
Imesainiwa na:
[DHAHIRI A.
KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA
WA POLISI MKOA WA MBEYA.

0 Comments