Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar
.....................................
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwanaharakati Bibi Siti bint Saad, Bi Nasra Moh’d Hilali amewataka wanawake kushikamana kwa pamoja kupinga udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto .
Kauli hiyo ameitoa
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisi kwake ndani ya Wizara ya
Habari Utalii Utamaduni na Michezo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema
udhalilishaji wa kijinsia umekithiri katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar jambo ambalo
linapelekea kudhoofisha maendeleo nchini hivyo amewashauri akinamama kupiga
vita vitendo hivyo .
Katika kupambana
na vitendo hivyo Bi Nasra ameitaka jamii
kujenga mashirikiano ya pamoja katika mfumo mzima wa malezi ya watoto na kuona watoto ni wa jamii
na sio ya wazazi wawili pekee.
“Tujiunge kwa pamoja tuseme hatutaki udhalilishaji na tusiiachie Serikali pekee kwani suala hilo ni
kubwa na linaathiri watu wengi kisaikolojia,”alisema Bi. Nasra
Alieleza
tukio la hivi karibuni la mwanamke kuchomwa
moto na mpenzi wake katika kijiji cha
Paje linaonyesha udhalilishaji uliokithiri
katika jamii na kuchangia kupoteza nguvu kazi ya taifa.
Alifafanua kuwa
kauli mbaya wanazotoa wanaume kwa wake
zao zinachangia udhalilishaji uliowazi na amewataka akinababa kuwa na kauli
nzuri kwa familia zao.
Aidha aliwataka akinamama kuwa tayari
kutoa taarifa wanapobaini dalili
za mtoto wa jirani anataka
kudhalilishwa ili hatua za kuzuia
vitendo hivyo ziweze kuchukuliwa kwa haraka.


0 Comments