WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema atamuita Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Bw. Hassan
Jarufo ili aje amueleze ni kwa nini wakulima wa zao hilo wanacheleweshewa
malipo yao kinyume na maagizo ya Serikali.
Ametoa kauli
hiyo leo mchana wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Lndi
mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa huo kwenye Ikulu ndogo wilayani Nachingwea.
Waziri Mkuu amewasili wilayani Nachingwea akiwa njiani kuelekea Ruangwa kwa mapumziko
ya mwisho wa mwaka.
“Niliagiza
wanunuzi waje na bond (dhamana ya mauzo), waziweke benki ndipo waingizwe kwenye
mnada. Kwa maana hiyo mnada ukimalizika, benki inakata fedha husika na kuingiza
kwenye chama cha wakulima.”
“Hapa tatizo
ni kwamba hatukusimamia vizuri zuala hili. Tulipaswa tujiridhishishe kwanza
kama mnunuzi amelipa fedha benki. Tatizo la biashara hii watu wengi ni
madalali, wanaangalia hali ikoje na wakibaini kuna cha juu, ndiyo anaagiza na
kuamua kuja kulipa. Kama angekuwa amelipa benki, ile hela ya awali ingekatwa
katika fedha ya dhamana aliyokwishaitoa,” amesisitiza.
Oktoba
16, 2016 wakati
akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja cha
Sokoine wilayani Nachingwea, mkoani Lindi, Waziri Mkuu
alisema alishatoa maelekezo tangu Aprili, mwaka huu kwamba wanunuzi wa korosho
ni lazima watoe asilimia 25 ya malipo wanayotaka ili kuepuka tatizo la madalali
kuingilia kati biashara hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa
Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi na Wakuu wote wa wilaya za mkoa huo wawahimize
wakulima wapande miche mipya ya korosho kwa sababu mikorosho iliyopo imezeeka
na haitoi mazao ya kutosha.
“Mnatakiwa
muwahimize wananchi wapande miche mipya mara tu mvua zitakapoanza ili ianze
kukua wakati wakusubiria kung’oa ile ya zamani. Nimeambiwa korosho bora
hazipaswi kuzidi punje 190 ili zijae kwenye kilo moja. Ubora wa miti ya korosho ukishuka na
idadi ya punje pia inapungua,” amesema.
Amesema
kigezo kikuu cha ununuzi wa korosho hivi sasa ni idadi ya punje na kwa Ruangwa
na Nachingwea, idadi inakuwa kubwa kwa sababu punje zake ni ndogo. “Wenzetu wa
Tandahimba walipanda miche mipya tangu miaka minne iliyopita kwa hiyo sasa hivi
wanavuna korosho zenye ubora,” ameongeza.
Amempongeza
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba kwa uamuzi wake wa
kuvunja mfuko wa wakfu wa korosho (CIDTF) na akamtaka afute mifuko kama hiyo
kwenye mazao mengine kama katani, chai na kahawa kwani inafanya kazi ambazo
zinaweza kufanywa na bodi za mazao hayo.
“Waziri
Tizeba alishaanza na zao la pamba, sasa aende kwenye mazao mengine ili fedha
ambazo watu wa mfuko huu walikuwa wakizitumia kulipana posho tu, sasa ziende
kwenye bodi kuhamasisha wakulima walime zaidi na ikibidi wapewe hata mashine za
kupulizia dawa,” ameongeza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, DESEMBA 27, 2016.
No comments:
Post a Comment