WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewashukuru na kuwapongeza madaktari wa Taasisi ya Bilal Muslim Tanzania
ambayo imetoa huduma ya matibabu ya macho kwa zaidi ya wananchi 4,000 wa mkoa
wa Dodoma
Ametoa pongezi hizo jana usiku (Jumapili
, Desemba 11, 2016) wakati akizungumza na madaktari waliotoa huduma hiyo
walipomtembelea katika makazi ya Waziri Mkuu mkoani Dodoma
Waziri Mkuu alisema huduma wanayoitoa
ni muhimu kwa kuwa imewezesha watu ambao walikata tamaa ya kuona wameona, hivyo
aliwaomba waendelee kwenda katika maeneo mengine nchini ili Watanzania wengi
zaidi waweze kunufaika.
"Nawashukuru kwa mchango mkubwa
mnaoutoa katika kuunga mkono jitihada za Serikali kwenye utoaji wa huduma za
matibabu ya macho bure na kuwawezesha hata wale wasiokuwa na uwezo kupata
huduma ," alisema .
Serikali ya awamu ya Tano ina
dhamira ya dhati kuwatumikia wananchi na kutoa huduma kwa wote , hivyo tuko
tayari kushirikiana na taasisi yeyote
ambayo inakusudia kuwafikia wananchi.
Waziri Mkuu alisema “katika utoaji
huduma za jamii , Serikali inathamini sana mchango wa taasisi binafsi na za
dini ambazo ziko mstari wa mbele kushirikiana na jamii kwa ujumla,”.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
aliwakaribisha madaktari hao kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali mkoani
Dodoma. “Hapa ndio makao makuu ya Tanzania , hivyo nawakaribisha mje kuwekeza,
ardhi ya kutosha ipo . Mnaweza kuja kujenga hospitali kubwa ya macho," alisema
.
Naye Naibu wa Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana na Ajira, Mheshimiwa, Anthony Mavunde alisema jumla ya watoto 250 wamefanyiwa
upasuaji wa macho na madaktari hao ambao walianza kutoa huduma hiyo
Desemba 8, 2016 na wanatarajiwa kumaliza Desemba 12, 2016
"Nawashukuru kwa moyo wenu wa kujitolea
kuja kusaidia watu wenye mahitaji ya matibabu ya macho . Mkoa wa Dodoma
una changamoto kubwa ya matatizo ya macho .Nimefarijika sana kuona baadhi ya akinamama waliokuwa wamekata tamaa ya
kuona wameweza kuona tena,” alisema.
Naye Mtaribu
wa taasisi hiyo, Noorelain Sharrif alimuahidi Waziri Mkuu kwamba wataendelea kushirikiana
na Serikali katika utoaji wa huduma za matibabu ya macho bure kwa wananchi
wenye mahitaji na wako tayari kwenda popote nchini kutoa huduma hiyo
“Tuko tayari
kushirikiana na Serikali katika kutimiza wajibu wetu kwa jamii , tutafanya
hivyo wakati wowote na kwa wananchi wote,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, DESEMBA 12, 2016.

0 Comments